Mtasubiri ft Zuchu na Nyimbo Zingine za Diamond Platnumz Zilizofungiwa Tanzania
11 May 2022
[Picha: YouTube]
Mwandishi: Charles Maganga
Pakua Ngoma Zake Nandy Bila Malipo Kwenye Mdundo
Kwa muda sasa, msanii Diamond Platnumz amekuwa akilalamika mara kwa mara kuhusu mamlaka zinazohusika na sanaa nchini Tanzania kufungia nyimbo zake. Kwa nyakati tofauti tofauti, Baraza La Sanaa la Taifa yaani BASATA pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania yaani TCRA wamekuwa wakipiga marufuku nyimbo au video za Diamond Platnumz kupigwa kwenye TV na Redio nchini Tanzania kutokana na sababu mbalimbali ambazo huwa wanazitoa.
Free Download: Pakua mixes 7 Kali za Clouds FM ndani ya Mdundo
Zifuatazo ni ngoma tano za Diamond Platnumz ambazo zimeshawahi kufungiwa na mamlaka za nchini Tanzania:
Soma Pia: Tuzo za Muziki za MTV Afrika Kufanyika Tanzania Mwaka 2023
Waka
Machi ya mwaka 2018 haikuwa njema sana kwa Diamond Platnumz baada ya ngoma yake ya Waka ambayo alimshirikisha Rick Ross kufungiwa na BASATA. Pamoja na kwamba maelezo ya kujitosheleza hayakutolewa na Baraza hilo, video ya ngoma hiyo ambayo wasichana wanaonekana wakiwa wamevalia mavazi ya ufukweni na ya ‘faragha’ yanakisiwa kuchangia uamuzi huo.
Mwanza
Miaka mitatu iliyopita ngoma ya ‘Mwanza’ ya kwake Diamond Platnumz na Rayvanny ilifungiwa na BASATA kwa sababu ilitumia maneno ‘yasiyofaa’. BASATA walikataza, ngoma hii kuchezwa kwenye redio na TV na kwenda mbali zaidi kwa kuwataka Wasafi waitoe mitandaoni ikiwemo YouTube. Ngoma hii pia ilipelekea Diamond Platnumz kufungiwa kutumbuiza kwa muda baada ya kutumbuiza ngoma hii kwenye tamasha ilhali walikatazwa na Baraza hilo.
Hallelujah
Kufikia sasa bado haijawekwa wazi kwanini ngoma hii ya Hallelujah ambayo Diamond Platnumz aliwashirikisha Morgan Heritage ilifungiwa. Wengi wameshuku huenda video ya ngoma hiyo na mashahiri yake vikawa chanzo kwa ngoma hiyo kuwekwa ‘kabatini’ na BASATA.
Mtasubiri
Mamlaka ya TCRA ikishirikiana na BASATA walifungia video hii siku chache zilizopita, baada ya kusema kuwa baadhi ya vipande kwenye video hiyo vimekwaza na kukera waumini wa dini ya kikristo. Kipande hicho ambacho kinaonekana kwenye sehemu ya kwanza ya video kinamuonesha Zuchu akitoka kwenye mazoezi ya kwaya, kanisani na kupokea simu kisha kwenda kukutana na Diamond Platnumz ambaye aliigiza kama mpenzi wake. Baada ya video hiyo kufungiwa na TCRA Zuchu na Diamond Platnumz walitoa masononeko yao kupitia mitandao ya kijamiii ambapo Diamond Platnumz alitanabaisha kuwa vitendo kama hivyo ndivyo hupelekea yeye kutoshiriki tuzo zinazoandaliwa na BASATA.
Zigo Remix
Mwaka 2016 ngoma ya Zigo Remix ambayo Diamond Platnumz alishirikishwa na AY pia iliwekwa kabatini kutokana na baadhi vipande vya video hiyo kuonekana kukosa maadili. Ngoma ya Zigo Remix ilifungiwa kuonekana mchana na badala yake ilielekezwa kuwa, vyombo vya habari vicheze video hiyo muda wa usiku tu.
Wasanii wengine ambao wameshawahi kukutana na rungu la BASATA ni pamoja na Nay Wa Mitego, Jux pamoja na Snura kupitia ngoma yake ya kuitwa ‘Chura’
Leave your comment