Matukio 5 Kubwa Yaliyopamba Tanzania Music Awards 2021
5 April 2022
[Picha: Instagram]
Mwandishi: Charles Maganga
Pakua Ngoma Zake Nandy Bila Malipo Kwenye Mdundo
April 2 mwaka 2022 ulikuwa ni usiku wenye maana kubwa kwenye tasnia ya muziki nchini Tanzania baada ya kufanyika hafla ya ugawaji wa tuzo za muziki ikiwa ni miaka saba tangu tuzo hizo zisimame. Kuanzia kwenye mikato ya aina yake ya fasheni za wasanii kwenye uwanja wa zulia jekundu, mahojiano waliyofanya wasanii na vyombo vya habari usiku wa tuzo mpaka kwenye machozi ya furaha waliyotoa baadhi wasanii baada ya ushindi, itoshe kusema tu kuwa shughuli ya ugawaji tuzo ilifana sana.
Soma Pia: Nandy ‘Siwezi’, Diamond ‘Fine’ na Nyimbo Zingine Zinazovuma Bongo Wiki Hii
Ali Kiba aliibuka kidedea kwenye Tanzania Music Awards 2021 baada ya kubeba tuzo 5 akifuatiwa na Nandy, Harmonize pamoja na Sholo Mwamba ambao walibeba tuzo 3. Yafuatayo ni matukio makubwa matano ambayo yalipamba sana hafla ya Tanzania Music Awards 2021:
Marioo kutangaza jina la albamu yake
Baada ya kushinda tuzo ya msanii bora wa kiume Bongo Fleva kwa mwaka 2021, Marioo katika hotuba yake alisema kuwa albamu yake ambayo ipo mbioni kuingia sokoni itaitwa ‘The Boy You Know’ kitu ambacho kilizua shangwe kubwa kutoka mashabiki. Ngoma yake Marioo ya Bia Tamu pia ilishinda kama wimbo bora wa Bongo Fleva.
Free Download: Pakua Mixes 7 kali kutoka Tanzania za mziki wa Bongo, Singeli na Amapiano Tamu
Diamond Platnumz kupewa tuzo ya heshima
Ikumbukwe kuwa Diamond Platnumz pamoja na lebo nzima ya Wasafi hawakushiriki tuzo ambazo ziliandaliwa na Baraza la Sanaa Tanzania kwani hawakupeleka kazi zao kwa waandaaji ili waweze kupata teuzi. Liha ya kususia tuzo hizo, Diamond alitunukiwa tuzo ya heshima na waandaaji wa tuzo kwa mchango wake mkubwa katika kuinua muziki wa Tanzania ikiwemo kutangaza muziki wa Bongo Fleva kimataifa kitu ambacho kiliinua shangwe miongoni mwa wahudhuhuriaji wa tuzo hizo. Kando na Diamond Platnumz pia Rais Samia Suluhu Hassan, Jeshi La Ulinzi Tanzania, Marehemu Bi Kidude na Marehemu Ruge Mutahaba pia walipewa tuzo za heshima kwa mchango wao mkubwa kwenye muziki wa Tanzania.
Ushindi wa Young Lunya
Kipengele cha Hip-hop mara nyingi huwa ni kigumu sana kutokana na ushindani uliopo kwenye muziki wa Hip-hop hapa nchini Tanzania. Young Lunya alipobeba tuzo mbili kama msanii bora wa kiume Hip-hop pamoja na wimbo bora wa hip-hop wa mwaka, wengi sana walifurahi. Ushindi wa Lunya ulipigiwa makofi na wengi kwani aliwekwa na magwiji wa Hip-hop kama Profesa Jay, Darasa, Rapcha na Nay Wa Mitego.
Hotuba ya Harmonize Harmonize aliweza kuibuka mshindi wa tuzo tatu usiku huo, ambazo ni mtumbuizaji bora wa kiume, msanii bora wa kiume wa mwaka pamoja na Collabo bora ya kimataifa kupitia ngoma yake ya Attitude. Kila mara alipokuwa jukwaani, hakusita kumtaja mpenzi wake wa zamani wa kuitwa Kajala Masanja. Harmonize kwa sasa yuko kwenye harakati za kumrudisha mpenzi wake Kajala kwani mara kwa mara kupitia akaunti yake ya Instagram amekuwa akimuomba msamaha muigizaji huyo na kumtaka warudiane. Harmonize aliweza kuchangamsha tuzo hizo kwani kila alipokuwa anapanda kutoa hotuba alitumia fursa hiyo kumtaka Kajala amrudie ili wawe tena pamoja, kitu ambacho wengi walionekana kukifurahia kwa usiku huo.
Siasa kwenye tuzo
Wasanii wengi walipoenda kuchukua tuzo kwenye jukwaa walionekana kupongeza sana serikali hasa Rais Samia kwa kurudisha tuzo hizo, kitu ambacho baadhi ya watu mtandaoni walionekana kushangazwa nacho. Rapa Roma Mkatoliki pia alionekana kutopendezwa na suala hilo na hivyo akatumia akaunti yake ya Twitter kuandika: "Artist unashinda tuzo ya muziki,toa speech mshukuru producer,shukuru label, management, family, media house & fans! Haya mambo unapanda unaishukuru serikali, unamshukuru mama mheshimiwa, aah mimi sioni kama ni sawa bwana! mnawapa mizigo isiyo ya kwao!! kama nakosea niueni," aliandika Roma.
Leave your comment