Mbinu Zinazotumika na Wasanii wa Tanzania Kupeleka Bongo Fleva Kimataifa

[Picha: Pulse Live Kenya]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Ukiweka kando nchi kama Nigeria na Afrika Kusini, ukweli ni kuwa Tanzania ni mojawapo ya nchi ambayo kiwanda chake cha muziki kiko vizuri sana hapa barani Afrika na ugaibuni. Ukitazama kwa umakini , utagundua kuwa kwa miaka ya karibuni ni kama milango ya Bongo Fleva imefunguka zaidi kwani Rayvanny ana tuzo ya BET, Harmonize anajulikana sana nchini Nigeria, Nandy anafanya collabo na wasanii wakubwa kama Koffi Olomide na hata Diamond Platnumz nae kila siku anaweka rekodi mpya kwenye mtandao wa YouTube.

Pakua nyimbo za Marioo Bila Malipo Kwenye Mdundo

Wasanii hao tajwa na wengineo wengi kutoka Tanzania wamekuwa wakitumia njia mbalimbali kuhakikisha kuwa muziki wa Bongo Fleva hauishii tu nyumbani bali unaenda kwenye ngazi za kimataifa zaidi. Zifuatazo ni njia tano ambazo wasanii watanzania wametumia kufikisha Bongo Fleva kimataifa.

Soma Pia: Jinsi Bongo Fleva Imebadilika Miaka Kumi Iliyopita

Collabo za kimataifa

Diamond Platnumz yuko vizuri sana kwenye hii idara kwani ukimuweka kando Wizkid, Diamond Platnumz tayari ameshafanya kazi na wasanii wengi wakubwa Afrika na America kuanzia Alicia Keys, Rick Ross, Ne-Yo, Davido, P Square, Tiwa Savage, Burna Boy, Fally Ipupa na wengineo wengi. Hii imesaidia sana kufikisha muziki wetu sehemu mbalimbali duniani na kupata mashabiki wapya na ndio maana ‘Yope Remix’ ambayo amefanya na Innos B kutokea Congo ndio ngoma iliyotazamwa zaidi Afrika Mashariki kufikia sasa kwenye mtandao wa YouTube.

Kufanya Video Kali

Director Justin Campos kutoka Afrika Kusini ni shuhuda kuwa Vanessa Mdee alitumia takriban dola za kimarekani 20,000 ili kutengeneza video yake ya ‘Never Ever’ ya mwaka 2015. Na mara tu baada ya video hii kutoka, iliweza kutikisa kila upande wa Afrika. Wasanii wa Tanzania wamekuwa wakifanya video nzuri na za gharama ili video hizo ziweze kuchezwa kwemye vituo vya muziki vya nje kama Trace, Channel 0, MTV Base na nyinginezo. Hii inasaidia kujiongezea mashabiki wa nje ya nchi.

Kujaribu aina mpya ya muziki

Wasanii wengi wa kizazi kipya cha Bongo Fleva huwa ni kama wakulima hawachagui jembe. Wanafanya muziki kutokea mataifa mengine ili kuweza kuwavuta zaidi mashabiki wa nchi hizo. Hii inaeleza kwanini Rayvanny alifanya Kazomba kwenye ‘My Number One’, Amapiano kwenye ‘Chawa’ na Afro Fusion kwenye ‘Slow’.  Lengo ni kuvuta mashabiki wa nchi mbalimbali.

Kuwekeza kwenye mitandao ya kijamii

Ukweli ni kuwa wasanii wengi wa Tanzania wanatumia vizuri sana mitandao ya kijamii ili kuweza kufikisha kazi zao kimataifa. Diamond Platnumz ni mzuri sana kwenye hili suala kwani mara nyingi huepuka kufanya mahojiano na vyombo vya habari na hutumia akaunti yake ya Instagram yenye wafuasi takriban Milioni 14 kuhusu kazi zake anazotaka kuziachia. Kupitia mitandao ya kijamii, wasanii hutoa taarifa kwa watu wengi zaidi ambao wako ndani na nje ya nchi.

Kujifunza kiingereza

Unawezaje kuongea na wasanii wa nchi nyingine duniani kama hujui kiingereza? Hii inaeleza kwanini wasanii wengi wa lebo ya WCB hupata mafunzo ya lugha ya kiingereza mara tu wanapojiunga na lebo hiyo. Rayvanny aliingia WCB alikuwa hajui kiingereza lakini chini ya usimamizi wa Diamond Platnumz, aliweza kupikwa vyema kwenye lugha hiyo na ndio maana aliweza kuongea na wasanii wakubwa duniani kama Fat Joe pindi alipohudhuria tuzo za BET mwaka 2017.

Kujiunga na taasisi kubwa za muziki za duniani

Mwaka 2020 msanii Diamond Platnumz alijiunga rasmi na taasisi ya Recording Academy ambayo ni maarufu sana duniani kote kwa kuandaa tuzo za Grammy za huko nchini Marekani. Diamond Platnumz kujiunga na Recording Academy kulisaidia sana msanii huyu kuweza kutambulika kimataifa kwani miezi kadhaa baada ya kuwa mwanachama wa taasisi hiyo , goma mbili kutoka kwa Diamond yaani ‘Jeje’ pamoja na ‘Baba Lao’ zilichaguliwa kuwania tuzo hizo za Grammy kwa mwaka 2021.

Leave your comment