Jinsi Bongo Fleva Imebadilika Miaka Kumi Iliyopita
24 February 2022
[Picha: Music in Africa]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram
Kama unafuatilia muziki wa Bongo Fleva, bila shaka utakuwa ni shahidi kuwa kwa miaka 10 iliyopita, kiwanda hiki cha muziki kimebadilika sana. Ni ukweli kuwa kiwanda cha Bongo Fleva ambacho anahudumu Ibraah, Marioo, Zuchu au Mac Voice sasa hivi ni tofauti mno na kile ambacho Marlaw, Z Anto, Jay Mo au Sugu walikuwa wanatamba nacho.
Pakua Nyimbo za Mac Voice Bila Malipo Kwenye Mdundo
Mambo yamebadilika kuanzia namna ambavyo wasanii wanarekodi nyimbo mpaka namna ambavyo mashabiki wanasikiliza nyimbo hizo. Makala hii inaangazia maeneo 8 yanaoonesha utofauti wa Bongo Fleva ya sasa na kiwanda cha Bongo Fleva cha zamani:
Gharama za video
Ukweli ni kuwa zamani wasanii watanzania walikuwa hawawekezi pesa nyingi sana kwenye video za muziki. Ngoma zao zilikuwa ni kali ila ilikuwa ni ngumu sana kumshawishi msanii awekeze mamilioni yake kwenye video. Angekuuliza hela zote hizo za nini? Kila kitu kilibadilika mwaka 2013 baada ya Diamond Platnumz kuachia video yake ya ‘My Number One’. Hapo ndipo wasanii wengine kama Chegge, Navy Kenzo, Shetta, Madee na Vanessa Mdee ambaye alitumia takriban Milioni 40 za kitanzania kutengeneza video yake ya ‘Never Ever’, walianza kutumia pesa nyingi kugharamia video zao za muziki. Sasa hivi, wasanii wanawekeza pesa nyingi katika kuandaa video za kufana.
Pakua Nyimbo za Navy Kenzo Bila Malipo Kwenye Mdundo
Umuhimu wa lebo za muziki
Tofauti na zamani ambapo wasanii kama Marlaw, Z Anto, Jay Mo au Sugu waliweza kufanya vizuri bila kuwa chini ya lebo yoyote ya muziki, kwa sasa umuhimu wa lebo kwa msanii haukwepeki. Kwa sasa lebo zimekuwa nyingi Tanzania ikiwemo WCB, Rooftop, Konde Music Worldwide, Too Much Money na King's Music na zimehusika kupika wasanii wakubwa nchini Tanzania kama Zuchu, Whozu, Anjella, K2GA na wasanii wengine wengi.
Soma Pia: Vitu Muhimu Wasanii wa Bongo Wanafaa Kujua Kabla ya Kujiunga na Lebo za Muziki
Nguvu ya mitandao ya kijamii
Ukiweka kando kiki, kitu kingine ambacho wasanii wa zamani walikosa ni mitandao ya kijamii ambayo ilianza kuwa maarufu sana Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 2010. Kwa sasa, ni kama mitandao ya kijamii hasa Instagram na Facebook imechukua nafasi ya redio na TV. Hii ndio maana mara zote Whozu kazi zake husikika zaidi huko Tiktok, Roma Mkatoliki hakauki huko Twitter huku Diamond Platnumz akiwa ameweka ufalme wake huko Instagram akiwa na wafuasi takriban Milioni 14.
Kuwepo kwa mitandao ya kuuza na kutiririsha muziki
Zimeshapita zile zama ambazo albamu ilikuwa inanunuliwa kwenye CD na kanda au ili uweze kusikiliza ngoma ya Chidi Benz ni lazima uangalie TV na kusikiliza redio. Kuanzia mwaka wa 2013 kuja mbele, wasanii wengi walishtuka kuwa kuna mitandao kama YouTube au Mdundo ambapo wanaweza kuweka ngoma zao na kupata pesa nyingi. Wasanii kama Diamond Platnumz ambaye alianza zamani safari yake ya YouTube mwaka 2011 sasa anakula matunda tu ya safari yake hiyo. Yeye ndio msanii aliyetazwa zaidi kwenye YouTube barani Afrika.
Kukua kwa hadhi ya watayarishaji wa muziki (producers)
Ziara ya mtayarishaji wa muziki S2kizzy ya kuitwa ‘Pluto World Way Drift’ ambayo alisafiri kwenye nchi mbalimbali Africa kama Africa Kusini na Kenya ni uthibitisho tosha kuwa sasa hivi watayarishaji wa muziki wanapata pesa zaidi na heshima kuliko zamani. Tusisahau kuwa mtayarishaji wa muziki Abbah Process pia alishawahi kutoa albamu yake mwenyewe ya kuitwa ‘The Evolution’ ambayo imesheheni majina makubwa kama Darassa, Harmonize, Lavalava, Young Dee, Nandy, Marioo na Ruby kitu ambacho hakikuwahi kufanyika hapo mwanzo.
Matumizi ya ladha nyingine za muziki
Wasanii wa sasa hivi hawachagui aina gani ya muziki wafanye na ndio maana Marioo aliweza kufanya Amapiano kwenye ‘Bia Tamu’ na ‘Mama Amina’ kisha alibadilika kwenye ‘For You’ kwa kuimba muziki aina ya kazomba kisha kwenye ngoma ya ‘Wow’ pia Marioo alitumia vionjo vya Afro Pop. Siku hizi Bongo Fleva haina mipaka kama zamani ambapo msanii kama Marlaw alijikita zaidi kufanya muziki wa Bongo Fleva tu njia ambayo wasanii wa sasa kama Zuchu, Whozu, Lavalava na hata Anjella wamegoma kupita kwani mara zote wasanii wa sasa hujaribu kuleta ladha mpya kwenye muziki.
Muziki kwenda kimataifa
Kwa sasa, muziki wa Bongo Fleva haufanyiki ‘chumbani’ tena bali milango imeanza kufunguka na wasanii Tanzania wanafahamika hata nchi nyingine hapa Afrika. Shukran nyingi sana ziwaendee wasanii kama Diamond Platnumz, Harmonize, Ali Kiba, Vanessa Mdee, Navy Kenzo, Rayvanny, Nandy na wengineo wengi ambao wameupigania muziki huu uvuke mipaka. Rayvanny kushinda tuzo ya BET, Nandy kutumbuiza kwenye tuzo za Afrimma pamoja na Diamond platnumz kuingia mkataba na kampuni ya Warner Music Group ya nchini Marekani ni baadhi ya viashiria kuwa sasa Bongo Fleva inafika kimataifa.
Leave your comment