TID Atangaza Kuachia Ngoma ya Kwanza Kwenye Albamu Yake ya Sita

[Picha: TID Instagram]

Mwandishi: Brian Sikulu

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mkongwe wa muziki wa bongo TID ametangaza kuwa ataachia ngoma ya kwanza kwenye albamu yake ya sita mnamo tarehe sita mwezi huu wa Januari.

Ngoma hiyo imepewa jina la 'Macho' huku albamu ikipewa jina la 'Ni Yeye'. 'Macho' imetayarishwa na Mr. Simon ambaye ni mmoja kati ya watayarishaji wa muziki wanaotajika zaidi kwenye tasnia ya muziki wa Tanzania.

Soma Pia: Maua Sama Atoa Kauli Yake Kuhusu Wasanii wa Bongo Kufanya Amapiano

TID kwenye chapisho aliloliweka mtandaoni alisema kuwa nia ya kutoa ngoma hiyo ni kuuheshimisha muziki wa bongo. Huenda hili limetokana na mjadala ulioko mtandaoni kuwa muziki wa bongo umefifia.

"Mwaka huu nimeamua kurudisha heshima ya bongofleva ...Kutoka kwenye album ya sita #niyeye single ya kwanza kabisa #macho by TID produced by @mrsimonofficial inatoka alhamisi hii tarehe 6," chapisho la TID mtandaoni lilisomeka.

Soma Pia: Diamond, Rayvanny na Harmonize Waongoza Orodha ya Wasanii Wenye Wafuatiliaji Wengi Zaidi YouTube Afrika

Tangazo hilo lilipata mapokezi mazuri miongoni mwa wafuasi wake ambao walionyesha furaha na hamu ya kuiskiza kazi hiyo mpya.

TID ni mmoja kati ya wanamuziki waliotamba sana katika enzi ya zamani ya muziki wa bongo. Alipata umaarufu mkubwa kutokana na ngoma zake kama vile 'Nyota Yako', 'Siamini' pamoja na ngoma zingine.

Japo TID hajavuma sana kwenye muziki wa kizazi kipya, nafasi na mchango wake kwenye muziki wa bongo fleva ni ya kuheshimika mno. Mashabiki wanatarajia TID kuitetea nafasi yake mwaka huu kwa kutoa ngoma kali.

Leave your comment