Matamasha ya Muziki Tanzania Yaliyofanya Vizuri Zaidi Mwaka 2021
20 December 2021
[Picha: Nandy Instagram]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram
Kama kuna kitu amacho kilinogesha mwaka 2021 basi ni matamasha ya kimuziki ambayo yamekuwa kama chachu ya kukua na kuongezeka thamani kwa muziki wa Bongo Fleva. Yafuatayo ni matamsha matano ya kimuziki ambayo yameweza kufanya vizuri zaidi ndani ya mwaka 2021.
Soma Pia: Matukio 10 ya Kimuziki Yaliyopamba Bongo Mwaka 2021
Waukae Festival
Tamasha hili liliandaliwa na meneja wa Diamond Platnumz na mbunge wa Morogoro kusini Mashariki Hamisi Taletale na lilifanyika huko mkoani Morogoro katika kata ya Kiroka Agosti 12 mwaka huu. Tamasha hili lilifana sana kwani halikuhusisha wasanii wa WCB pekee bali pia wasanii wengine nje ya WCB kama Belle9, Dogo Janja, Queen Darleen, Mwana Fa, Billnass, Fid Q, AY, Afande Sele, Shilole, Chege na wengine wengi.
Komaa Concert
Tamasha hili lilifanyika Desemba 3 mwaka huu na liliandaliwa na kituo cha TV E na EFM. Komaa Concert lilivuta mashabiki wengi na kuweza kuweka historia baada ya Harmonize na Ali Kiba ambao ni wasanii mashuhuri kutoka Tanzania kutumbuiza kwenye tamasha hilo ambalo lilifanyika viwanja vya Tanganyika Packers jijini Dar Es Salaam.
Soma Pia: Collabo 10 Kali Kutoka Tanzania Zilizofanya Vizuri Zaidi Mwaka 2021
Zuchu Homecoming
Tarehe 21 mwezi Agosti mwaka huu Uwanja wa Amani huko Zanzibar Kulipamba moto kufuatia tamasha la Zuchu Homecoming ambalo mwanamuziki Zuchu aliliandaa kama namna ya kurudisha asante kwa watu wa Zanzibar. Zuchu hakufanya peke yake tamasha hili bali alisindikizwa na wasanii kama Jux, Mr Blue, Baba Levo, Chege, Gigy Money, Queen Darleen, Khadija Kopa, Dulla Makabila na wengineo wengi.
Nandy Festival
Hili ni tamasha ambalo limezidi kumheshimisha Nandy kwenye muziki wa Bongo Fleva. Kupitia tamasha hili, Nandy alizunguka mikoa tofauti tofauti kama Mwanza, Dodoma, Kigoma na Dar Es Salaam huku akisindikizwa na wasanii wakubwa kama Billnass, Moni, Weusi, Willy Paul, Mabantu na wengineo wengi. Kilichovutia zaidi kwenye tamasha hili ni Rais Samia Suluhu Hassan kumpigia simu na kumpongeza Nandy kipindi anatumbuiza mkoani Dodoma.
Ibraah Homecoming
Muda mfupi baada ya kurudi nchini kutoka Marekani, Ibraah alitangaza onesho lake la kimuziki. Onesho la Ibraah lilifanyika Novemba 27 mwaka huu kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona huko mkoani Mtwara. Kunogesha zaidi tamasha hili, Ibraah alitumbuiza kwenye jukwaa moja na wasanii kama Anjella, Country Wizzy, Amber Lulu, Killy, Barnaba na mwisho kabisa Harmonize aliibuka kwenye tamasha hilo bila taarifa kitu ambacho kiliinua hisia za mashabiki.
Leave your comment