Matukio 10 ya Kimuziki Yaliyopamba Bongo Mwaka 2021

[Picha: Pulse Live]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Kama kuna mwaka kwenye muziki wa Bongo Fleva ambao umekuwa na matukio mengi na ya kusisimua, basi mwaka 2021 waweza kuwa unaongoza. Huu ni mwaka ambao kuna wasanii waliovunja rekodi mbalimbali, wasanii waliotoa albamu kali, ufunguzi wa lebo na mambo mengine mengi.

Soma Pia: Nyimbo Mpya: ‘Sukari’ Zuchu, ‘Baikoko’ Mbosso na Video Zingine kutoka Bongo Zilizotazamwa Zaidi YouTube Mwaka wa 2021

Yafuatayo ni matukio 10 yaliyotikisa kiwanda cha muziki nchini Tanzania kwa mwaka 2021:

Diamond Platnumz kuwania tuzo ya BET

Baada ya upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati wa kisiasa, taifa zima la Tanzania lilizima Juni 28 mwaka huu, ili kufahamu kama Diamond Platnumz atashinda tuzo ya BET kipengele cha msanii bora kutokea Africa. Licha ya kupoteza tuzo hiyo mbele ya Burna Boy, tukio hili liliunganisha sana wasanii wa Tanzania kwani wasanii wengi kama Jux, Shilole, Zuchu na wengineo walijitokeza kumuunga mkono msanii huyo.

Utambulisho wa Mac Voice

Ilipofika mwezi Septemba, Rayvanny alimtambulisha msanii wa kwanza wa lebo yake ya Next Level Music wa kuitwa Mac Voice.  Ujio wa Mac Voice ulizungumziwa haswa na vyombo vya habari kutokana na Mac kuwa msanii wa kwanza kutambulishwa na Rayvanny. Hii ilipelekea EP ya kinda huyo inayoitwa ‘My Voice’ kufanya vizuri sana.

Soma Pia: Diamond, Nandy na Director Kenny Wang'aa Kwenye Tuzo Za Afrimma

Uzinduzi wa albamu ya Ali Kiba ‘Only One King’

‘Only One King’ ni moja kati ya albamu zilizosubiriwa kwa muda mrefu sana. Oktoba 6 ambayo ilikuwa ni siku ya uzinduzi  wa albamu hiyo, takriban watu Milioni 1 walikuwa wakifuatilia tukio kwenye mtandao wa YouTube, huku wasanii kama Ommy Dimpoz, Nandy, AY, Mwana FA pia wakihudhuria hafla hiyo.

Tamasha la Zuchu Homecoming

Mwishoni mwa mwezi Agosti Zuchu aliweza kuchangamsha visiwa vya Zanzibar sehemu ambayo amezaliwa, kwa tamasha lake la ‘Zuchu Homecoming’. Tamasha hili lilinoga zaidi kwani Zuchu alisindikizwa na wasanii wakubwa kutoka bara  kama Mbosso, Jux, Mr Blue, Gigy Money, Lulu Diva na Dulla Makabila.

Tangazo la Rais Samia kuhusu mirabaha kwa wanamuziki

Mwezi Juni mwaka huu Rais Samia alitangaza azimio la kuanzisha mfumo wa kuwalipa wasanii pindi nyimbo zao zinapochezwa kwenye redio na TV. Tangazo hili liliibua hisia tofauti kwa wanamuziki kwani wengi wao kama Wakazi, AY na Mwana FA walionekana kuunga mkono mfumo hao. Wasanii wengine haswa wale wachangaa waonyesha kuwa na wasiwasi kuwa ngoma zao huenda zisipate nafasi kabisa kwenye vyombo vya habari.

Rayvanny kutumbuiza kwenye tuzo za  MTV EMA

Mwezi Novemba mwaka huu, Rayvanny aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kutokea Tanzania na Afrika kwa ujumla kutumbuiza kwenye tuzo za MTV Europe Music Awards ambapo alitumbuiza wimbo wa ‘Mama Tetema’ akiwa na msanii kutokea Columbia Maluma.

Hanstone na sakata la WCB

Baada ya tetesi za muda mrefu kuwa mwanamuziki Hanstone yuko chini ya usimamizi wa lebo ya WCB, hatimaye mwezi Oktoba mwaka huu alinyamazisha tetesi hizo baada ya kuachia EP yake ya ‘Amaizing’ kwenye mitandao ya kutiririsha muziki. Mara baada ya EP hiyo kutoka, mashabiki wengi wamekuwa wakihoji hatma ya msanii huyo na Oktoba 19 mwaka huu, Baba Levo ambaye ni mtu wa karibu na Diamond Platnumz alitanabaisha kuwa Hanstone aliamua kujiweka kando na Wasafi kwani alikosa uvumilivu.

Anjella kujiunga Konde Gang

Mwanzoni mwa mwaka huu, Harmonize kwa mara ya kwanza alimtambulisha msanii wa kike Anjella kwenye lebo yake ya Konde Gang. Habari hii ilipamba vichwa vya habari nchini Tanzania kutokana na ukubwa wa lebo hiyo nchini.

Bifu la Roma Mkatoliki na Nikki Mbishi

Rapa Roma Mkatoliki aliamua kumtolea uvivu rapa Nikki Mbishi baada ya Nikki Mbishi kusema kuwa Roma alipata umaarufu baada ya kutekwa mwaka 2017 akiwa na Moni Centrozone. Roma aliandika kupitia akaunti yake ya Instagram kuwa Nikki Mbishi ajikite zaidi kwenye muziki wake badala ya kujihusisha na maisha ya wasanii wengine.

Tamasha la Nandy Festival

Kama kuna tamasha la muziki lililofanya vizuri kwa mwaka huu basi ni Nandy Festival ambapo Nandy alizunguka mikoa tofauti tofauti kama Mwanza, Arusha, Dodoma na Dar Es Salaam huku akisindikizwa na wasanii kama Billnass, Rosa Ree, Professor Jay na wengineo wengi.

Leave your comment