Wasanii 10 Bora Tanzania Kwa Mwaka 2021
16 December 2021
[Picha: Music in Africa]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram
Kama unapenda muziki kutokea nchini Tanzania, basi bila shaka utakuwa pia unawafahamu na kuwakubali wasanii tofauti tofauti ambao kutokana na kazi zao wamezidi kuijenga na kuimarisha himaya ya muziki wa Bongo Fleva. Wafuatao ni wasanii 10 bora ambao wameweza kufanya vizuri sana kwa mwaka 2021.
Rayvanny
Hakuna mwaka ambao Rayvanny ameachia kazi nyingi kama 2021. Hii ni baada ya kuachia ‘Sounds From Africa’ albamu iliyosumbua sana nchini Tanzania na mwezi Oktoba aliachia EP yake ya ‘New Chui’ ambayo pia ilipokelewa kwa mikono miwili na mashabiki. Rayvanny pia alipata kufanya kazi na Mlamu kutoka Columbia.
AliKiba
Huu ulikuwa ni mwaka ambao Alikiba ameweza kuufikisha muziki wake kimataifa baada ya kufanya ngoma na wasanii mbalimbali wa kimataifa kama Rude Boy, Patoranking, Mayorkun, Sarkodie, Nyashinski na Sauti Sol kupitia albamu yake ya ‘Only One King.
Soma Pia: Matukio 10 ya Kimuziki Yaliyopamba Bongo Mwaka 2021
Mbosso
Kwa mwaka huu, Mbosso alikuwa na silaha moja tu, nayo ni albamu yake ya ‘Definition of Love’. Albamu hiyo ina ngoma tofauti tofauti ambazo zilichangamsha taifa. Ngoma kubwa kabisa kwenye albamu hiyo ilikuwa ni ‘Baikoko’ ambayo imeweka rekodi ya kuwa video ya muziki ya pili kutazamwa zaidi YouTube Tanzania kwa mwaka wa 2021.
Nandy
Ndani ya mwaka huu, Nandy ameachia EP mbili ambazo ni ‘Wanibariki’ pamoja na ‘Taste’. Zote zimeweza kufanya vizuri. Tamasha lake la Nandy Festival kwa mwaka 2021 limezidi kuwa kivutio kikubwa huku video ya ngoma yake ya ‘Nimekuzoea’ ikiwa ndo video ya tatu ya iliyotazamwa zaidi kwa msanii wa kike kutoka Tanzania mwaka huu.
Diamond Platnumz
Kwa mwaka 2021, Diamond Platnumz ameachia ngoma tano ambazo zote zimeweza kufanya vizuri. Huu ni mwaka ambao Diamond Platnumz amejaribu aina ya muziki tofauti kwani ameimba Kizomba kwenye ‘Naanzaje’, Afro Pop kwenye ‘Kamata’ pamoja na ‘Gimmie’ na Amapiano kwenye ‘Iyo’.
Soma Pia: Nyimbo Mpya: Albamu na EP 10 Kali Zaidi Tanzania Kwa Mwaka 2021
Jay Melody
Orodha hii isingekamilika bila kumtaja Jay Melody ambaye kwa mwaka huu aliweza kutufanya tucheze dansi kupitia ngoma yake ya ‘Huba Hulu’. Kuna tetesi kuwa Rayvanny na Ali Kiba wote wako tayari wameshafanyia remix ngoma hiyo. Ngoma nyingine kutoka Jay Melody zilizokita ni ‘Najieka’ ya mwezi Juni pamoja na ‘Halafu’ na ‘Sambaloketo’ ambazo ziliachiwa mwezi wa Agosti.
Zuchu
Ndani ya mwaka huu, Zuchu ameendelea kuweka rekodi mbalimbali ikiwemo video yake ya ‘Sukari’ kuwa video ya muziki iliyotazamwa zaidi kwa mwaka 2021 barani Afrika. Wimbo wake wa ‘Nyumba Ndogo’ pia imeweka rekodi mpya kwenye muziki wa singeli. Ukiachilia mbali tamasha lake la Zuchu Homecoming ambalo lilifanya vizuri sana, kwa mwaka huu, Zuchu ametajwa kuwania tuzo mbali mbali kama Afrima pamoja na AEUSA.
Marioo
Hakuna pingamizi lolote kuwa mwaka 2021 ni wa aina yake kwa Marioo. Kuanzia ngoma yake ya kwanza mwaka huu ‘For You’ ambayo imeweka rekodi mbalimbali kwenye mitandao ya kutiririsha muziki. Aidha ngoma yake ya ‘Bia Tamu’ imezidi kupaisha hadhi ya Marioo kama mfalme wa muziki wa Amapiano kwa hapa Afrika Mashariki.
Harmonize
Kuanzia onesho lake la kimuziki la huko nchini Marekani, kuteuliwa kuwania kwenye tuzo za Afrima pamoja na albamu yake ya ‘High School’ kusheheni ngoma zilizosumbua mitaa, Harmonize amekuwa na mwaka mzuri sana. Mojawapo ya rekodi kubwa ya Harmonize kwa mwaka huu ni pamoja na video yake ya ‘Attitude’ kutazamwa mara laki moja ndani ya dakika 44 tu kwenye mtandao wa YouTube.
Rosa Ree
Ndani ya mwaka huu, Rosa ametoa ngoma saba ikiwemo ‘Wana Wanywe Pombe’, ‘I'm Not Sorry’ na pia ‘Watatubu’. Kupitia ngoma hizi, waandaaji wa tuzo za Afrima waliona anastahili kuwania tuzo ya msanii bora wa Hip-hop barani Afrika. Licha ya kukosa tuzo, Rosa Ree amezidi kuimarisha nafasi yake kama malkia wa rap nchini Tanzania.
Leave your comment