Nyimbo Mpya: Albamu na EP 10 Kali Zaidi Tanzania Kwa Mwaka 2021

[Picha: Biggest Kaka]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Ukiweka kando tuzo za muziki za kimataifa na matamasha makubwa yaliyopamba tasnia ya muziki, kitu kingine ambacho kimechangamsha sana kiwanda cha muziki nchini Tanzania kwa mwaka 2021 ni EP na albamu zilizoachiwa na wasanii tofauti tofauti.

Soma Pia: Jinsi ya Kupata Hakimiliki ya Wimbo Nchini Tanzania

Kuanzia kwa wasanii wa Hip-hop, Bongo Fleva, RnB, Singeli na mitindo mbalimbali ya muziki, hakika mwaka 2021 ulifurika kwa albamu na EP. Nakala hii imelenga kuangazia albamu na EP 10 kali zaidi zilizoachiwa na wasanii wa Tanzania kwa mwaka 2021:

Sounds from Africa - Rayvanny

Rayvanny alifungua pazia la albamu kwa mwaka 2021 baada ya kuachia ‘Sounds from Africa’. Albamu hii ilikuwa na ngoma 23 za moto. Hii ni albamu ambayo Rayvanny ameonesha uwezo wake wa kufanya aina tofauti ya muziki kama Kazomba kupitia ‘Number One Remix’, amefanya Afro Beats na Joe Boy kwenye ‘Rotate’ pamoja na Bongo Fleva kwenye ‘Lala’.

Promise – Lava lava

Ilipofika mwezi Februari mwaka huu, Lava lava alitukumbusha kuhusu ufundi wake kwenye kutunga, kuandika na kuimba nyimbo za mapenzi kupitia EP yake ya ‘Promise’. EP hio ina nyimbo nne ambayo ndani yake Lava lava anaugulia maumivu ya makali ya mapenzi.

Only One King - Alikiba

Wakati wasanii wengine wakikimbilia kwenye Amapiano na aina mpya ya muziki kutoka nje, Alikiba alithibitisha kuwa yeye ndiye mfalme na muasisi wa Bongo Fleva kupitia albamu yake ya ‘Only One King’ yenye nyimbo 16. Chini ya uangalizi makini wa Yogo Beats, ‘Only One King’ imemleta Alikiba mpya ambaye ameweza kushirikiana na wasanii kama Rude Boy, Mayorkun, Sarkodie na wasanii wengine wengi.

Taste – Nandy

EP ya ‘Taste’ imesheheni ngoma nne zenye uzito wa kutosha. Kwenye EP hii, Nandy alitaka kuonesha kipawa alichonacho kwenye kuimba kwani hakumshirikisha msanii yeyote.

Amaizing – Hanstone

Mwezi Oktoba Hanstone aliachia ‘Amaizing’ EP ambayo imesheheni ngoma 6 ambazo Hanstone ameimba peke yake. Ukisikiliza ngoma kama ‘Boya’ na ‘Nimechoka’ zinaonesha kabisa kwanini Hanstone aliamua kuipa EP hii jina la ‘Amaizing"’ kutokana na uandishi mzuri uliotumika na kikubwa ni sauti ya kipekee ya Hanstone.

Definition of Love - Mbosso

Kama unatafuta maana ya neno mapenzi, basi huna budi kusikiliza albamu hii kutoka kwa Mbosso. Hii ni albamu ambayo haichoshi kwani unaweza kusikiliza ngoma ya kwanza mpaka ya 14 bila kuruka wimbo wowote. Mbosso aliwashirikisha wasanii wakubwa kama vile; Diamond Platnumz, Liya na Spice Diana.

 High School – Harmonize

Harmonize hakuangusha mashabiki baada ya kuileta ‘High School’ mwezi Novemba mwaka huu.Tofauti kabisa na ‘Afro East’, ‘High School’ ni albamu ambayo Harmonize amegusia sana maisha yake ikiwemo aliyekuwa mke wake Sarah, mahusiano yake na Kajala, ushindani uliopo kwenye muziki na mengineyo mengi.

My Voice - Mac Voice

Hakuna namna nzuri ambayo tungeweza kufahamu uwezo wa Mac Voice kwenye muziki kama asingeachia EP yake ya ‘My Voice’. Kuanzia kwenye ‘Nenda’; ngoma ambayo inafungua EP mpaka kwenye ‘Bora peke yangu’, Mac Voice ameonesha uwezo wake wa sauti na kuandika ngoma.

Wanangu 99 - Rapcha

Ni sahihi kusema kuwa albamu ya ‘Wanangu 99’ imemleta Rapcha mpya ambaye kando na kuwa na umri mdogo, mashahiri yake yanaonesha ukomavu wa hali ya juu na kugusa watu wa rika zote. Kupitia albamu hii yenye ngoma 10, Rapcha amegusia mada tofauti tofauti kama urafiki, mapenzi, maisha ya bosi wake majani na mambo mengine kibao.

Karata Tatu - Ibraah

Kama kuna mradi wa muziki ambao Ibraah ameimba kwa hisia na kwa umakini mkubwa basi ‘Karata Tatu’ EP iliyotoka mwezi Januari mwaka 2021 huenda ikawa inaongoza. Kupitia ngoma kama ‘Mapenzi’ na ‘Nimpende’, Ibraah alituonesha kuwa kipaji chake sio cha kawaida na ndo maana yuko chini ya Konde Music Worldwide mpaka sasa.

Leave your comment