Rapcha Afichua Sababu ya Kumshirikisha Saraphina Kwenye ‘Duminage’

[Picha: Citi Muzik]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Rapa kutokea Bongo Records Rapcha hatimaye ameweka wazi ni nini hasa kilichopelekea kumshirikisha mwanadada Saraphina kwenye ngoma yake ya hivi karibuni ya kuitwa ‘Duminage’.

‘Duminage’ ni ngoma iliyopikwa na JiniX6 na ni ngoma ya kuchezeka ambayo ndani yake Rapcha anaelezea hisia zake kwa mwanamke, huku Saraphina akisikika zaidi kwenye aya ya pili ya ngoma hii akinogesha kibao hiki kwa sauti yake ya kuvutia.

Soma Pia: Rapcha Azungumza Baada ya Profesa Jay Kumfananisha na Mangwair

Akizungumza kwenye kituo cha Times FM, Rapcha amefichua kuwa msanii wa kwanza ambaye alikuwa amewaza kumshirikisha ni Linah Sanga lakini kutokana na muingiliano wa ratiba, walishindwa kuingia studio na kurekodi ngoma hiyo.

"Mtu wa kwanza kabisa kumfikiria kwenye ngoma ilikuwa ni Linah ikawa nishamsikiliza hadi demo sasa tukawa tumepanga kwamba, tulikuwa Dodoma kwamba tukirudi Dar tutarekodi lakini tulivyorudi kila mtu tena akawa na ratiba nyingine kwa hiyo ratiba zikawa zimechanganyikana," alizungumza Rapcha.

Soma Pia: Tommy Flavour Azungumzia Kujipa Cheo cha Ufalme wa RnB

Rapcha alieleza kuwa wakati bado anatafutana na Linah ndipo akaona kipande cha video mtandaoni cha Saraphina akiwa anaimba na akavutiwa na sauti yake.

"Hapo katikati nikawa nimekutana na clip ya Saraphina, niliona clip yake nyingine tu alikuwa anaimba tu cover nilivyoona hiyo nikafuatilia page yake nikajua ni mshindi wa BSS nikajaribu kumreach nikafahamu meneja wake ni D'Fighter, nikaongea na D'Fighter nikamwambia kuna track hii hapa nataka kutisha na Saraphina tukakutana studio tukatisha," alizungumza Rapcha.

Kando na Rapcha, Saraphina kwa mwaka 2021 ameshirikiana na wasanii tofauti tofauti nchini Tanzania ikiwemo rapa Baddest 47 kwenye ‘Singo’ pamoja na Chege ambao wamefanya ngoma mbili ‘Kushki’ pamoja na ‘Sinsima’.

Leave your comment