Diamond Platnumz Ateuliwa Kuwania Tuzo za MTV EMA 2021

[Picha: Bella Naija]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki kutokea lebo ya WCB Diamond Platnumz ameendelea kupeperusha bendera ya Bongo Fleva, baada ya kupata uteuzi kwenye tuzo za MTV Europe Music Awards kwa mwaka 2021.

Diamond Platnumz amepata uteuzi huo kwenye kipengele cha msanii bora kutokea bara la Afrika. Diamond anawania tuzo hiyo pamoja na wasanii wengine tajika kama vile; Wizkid na Tems kutokea nchini Nigeria, Amaarae wa nchini Ghana pamoja na Focalistic wa huko Afrika Kusini.

Soma Pia: Diamond ‘Gimmie’, Lulu Diva ‘Kawaida’ na Nyimbo Zingine Mpya Zilizoachiwa Bongo Wiki Hii

Tuzo za MTV EMA huandaliwa na kampuni ya Viacom International Media Networks ambayo inamiliki vituo vya runinga vya MTV sehemu mbalimbali duniani kama Ulaya, Mashariki ya kati na Afrika.

Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika huko Budapest nchini Hungary tarehe 14 Novemba mwaka huu.

Diamond Platnumz sio mgeni wa kushiriki kwenye tuzo hizi kwani mwaka 2015 alishinda tuzo hii ya msanii bora kutokea Afrika akiibuka mshindi mbele ya wasanii kama Davido, Yemi Alade, AKA na DJ Arafat.

Soma Pia: Sababu Tano Kuu Zinazoeleza Mbona Tasnia ya Muziki ya Tanzania Inahitaji Tuzo Za Kinyumbani

Mwaka wa 2016, Alikiba alishinda tuzo hii ya MTV EMA mbele ya wasanii kama Olamide na Wizkid kutokea Nigeria na Black Coffee na Casper Nyovest kutokea Afrika Kusini.

Mwaka wa 2020, msanii kutokea Afrika Kusini ambaye alitetemesha dunia na ngoma yake ya ‘Jerusalema’ Master KG alishinda tuzo hii yenye heshima kubwa kwenye tasnia ya muziki.

Ikumbukwe kuwa kando na tuzo hii ya MTV EMA, Diamond pia ametajwa kuwania tuzo za AFRIMMA kwenye vipengele zaidi ya vine. Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika tarehe 14 Novemba.

Leave your comment