Sababu Tano Kuu Zinazoeleza Mbona Tasnia ya Muziki ya Tanzania Inahitaji Tuzo Za Kinyumbani

[Picha: THT]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Imeshatimia miaka 6 sasa tangu tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards, ambazo huandaliwa kwa ushirikiano na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kusitishwa. Tangu hapo, taifa hili lenye watu zaidi ya milioni 50 halijawahi kupata tuzo zozote za muziki.

Tangu mwaka 2015, wasanii wa Tanzania wameishia kudoea nafasi za tuzo kutoka mataifa mengine kama Soundcity (Nigeria), AEUSA (Marekani), na AFRIMA ambazo huandaliwa na Umoja wa Afrika (AU). Pamoja na ukweli kuwa tuzo hizi za kimataifa hupeperusha vilivyo bendera za Bongo Fleva huko duniani, lakini siku zote ‘Mcheza Kwao Hutunzwa".

Umuhimu wa tuzo kwenye muziki wa Tanzania ni mithili ya chumvi kwenye mboga ambayo kazi yake ni kuongeza ladha kwenye chakula. Makala hii inaangazia sababu kuu tano kwanini kiwanda cha muziki nchini Tanzania kinahitaji tuzo za muziki:

Soma Pia: Sababu Nne Kuu Zinazowafanya Wasanii Wengi Tanzania Kuanzisha Lebo za Muziki

  1. Tuzo zinaongeza hari na ushindani wenye afya baina ya wanamuziki

Baada ya watu kumkosoa Vanessa Mdee na kusema kuwa ngoma yake ‘Closer’ haikustahili kushinda wimbo bora wa RnB kwenye KTMA mwaka 2014, Vee Money alikaa chini na kuandika ngoma ya ‘Hawajui’ ili kujibu mapigo. Huu ni uthibitisho kuwa tuzo huleta hasira, hari na hamasa kwa wasanii ili wafanye kazi zenye viwango vya juu, na waweze kupata tuzo na kuongeza idadi ya mashabiki.

  1. Tuzo Hukuza thamani ya wasanii wachanga na kuwafanya kuwa wasanii wakubwa

Kabla ya kushinda tuzo ya KTMA mwaka 2013, Kala Jeremiah alikuwa anaonekana ni rapa wa kawaida tu. Kila kitu kilibadilika  baada ya kubeba tuzo ya  msanii bora wa Hiphop mbele ya manguli kama Stamina, Profesa J, Fid Q na Joh Makini. Hapo ndipo Kala alitambulika kama msanii mwenye hadhi yake kwenye uwanja wa Hiphop

Tuzo hukuza majina ya wasanii hasa wale wadogo wanaposhinda na kuwabwaga wasanii wakubwa. Leo hii kukiwa na tuzo na Mac Voice akamshinda Rayvanny au hata Madee, hadhi yake itapanda maradufu.

Soma Pia: Wasifu wa Anjella, Safari Yake Kimuziki, Nyimbo Zake Bora, Mafanikio, Mahusiano na Thamani Yake

  1. Tuzo hutengeneza historia ya kudumu kwa msanii

Msanii akipata tuzo fulani huishi nayo siku zote na ana uwezo hata wa kuonesha watoto wake kuwa ashawahi kushinda tuzo fulani. Hii ni tofauti kabisa ukishika namba 1 Trending YouTube kwani hupati tuzo yoyote. Ndio maana ukienda makao makuu ya Next Level Music, Rayvanny anajivunia bila tashwishwi kuonesha tuzo yake ya BET.

Kukosekana kwa tuzo kunatengeneza mastaa wengi ambao hata wakienda nchi za nje, wanashindwa kujisifu kuwa walishawahi kushinda tuzo fulani.

  1. Tuzo hukuza hadhi ya kiwanda cha Bongo Fleva kwa ujumla

Ukiweka kando Nigeria na Afrika Kusini, Tanzania inasifika sana kwa kuwa na kiwanda cha muziki kikubwa lakini sifa hii inaingia doa kwani hatuna tuzo zetu wenyewe ndani ya nchi. Kwa upande wa Nigeria wana tuzo zao kama Soundcity, The Headies na CPMA, Kenya wana tuzo za muziki za Kisima pamoja na Groove. Muziki wetu utaheshimiwa zaidi kama na Tanzania itakuwa na tuzo zake za muziki, ambazo pindi zikifanyika basi Afrika nzima itasimama kusikia washindi.

  1. Tuzo huinua na kutangaza zaidi tanzu (Genres) za muziki ambazo hazijajulikana

Tuzo hutangaza mitindo ya muziki ambayo watu wengi hawafuatilii kwa ukaribu kama vile taarab, muziki wa bendi, singeli, Zouk na hata Rhumba. Wengi walisikia majina ya waimba taarabu kama Mzee Yusuf, Isha Mashauzi na kuanza kuwafuatilia kwa ukaribu kazi zao kwenye msimu wa tuzo za KTMA. Hivyo basi, kukosekana kwa tuzo hapa nchini kumechagiza kudidimiza zaidi Taarab na muziki wa Bendi.

Leave your comment