Sababu Nne Kuu Zinazowafanya Wasanii Wengi Tanzania Kuanzisha Lebo za Muziki

[Picha: Diamond Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Kwenye kiwanda cha muziki hapa nchini Tanzania, suala la kuanzisha lebo ya muziki limekuwa ni jambo la kawaida tu. Ukiketi chini na wasanii kama Zuchu, Ibraah, Rosa Ree, Otuck William, Tommy Flavor na Brian Simba, bila tashwishwi watakubali kuwa lebo za muziki hasa zilizoanzishwa na wasanii wenye majina makubwa zina mchango uliotukuka katika kukuza sanaa zao.

Uwepo wa lebo kama WCB ya Diamond Platnumz, Makini Music ya Joh Makini, Konde Music Worldwide ya Harmonize, The Industry ya Navy Kenzo, Kings Music ya Alikiba, Mdee Music ya Vanessa Mdee na juzi juzi hapa Next Level Music ya Rayvanny ni ushahidi tosha kumekuwa na mwamko mkubwa sana wa wasanii kuanzisha kampuni zao binafsi za kusimamia wasanii.

Lakini nini kimechagiza mwamko huu? Hizi ni baadhi ya sababu:

Kushika Mkono Vipaji vya Wasanii Wachanga.

Wasanii wengi wakubwa huanzisha lebo ili kuwatangaza kiurahisi wasanii wapya ambao majina yao yalikuwa hayajulikani kabisa kwenye soko la muziki. Mathalan, wakati Ibraah anatambulishwa Konde Gang Aprili mwaka 2020,ni Harmonize ndiye alimtafutia Ibraah interviews kwenye vyombo vya habari vikubwa hapa Tanzania kama EFM, Clouds FM na hata Simulizi na Sauti.

Kukuza soko la muziki wa Tanzania kwa Ujumla.

Kiwanda cha muziki hunoga na kustawi zaidi pale ambapo wasanii wakubwa na wenye ushawishi wanaongezeka kila kukicha. Ndio maana Nigeria wanafanya vizuri sana Afrika kwa sababu wana wasanii wenye majina makubwa kama Davido, Burna Boy, Yemi Alade, Wizkid na wengineo. Kwa kutambua hilo, wasanii wengi watanzania huanzisha lebo ili kuongeza idadi ya wasanii wenye majina makubwa na watakaowakilisha Tanzania kimataifa. Mathalani, Zuchu kwa sasa ni mojawapo kati ya wasanii wakubwa Afrika Mashariki. Mwaka 2020 alishinda tuzo ya Afrimma kama msanii bora chipukizi barani Africa. Hii imechagizwa mno na uwepo wake kwenye lebo ya WCB ya Diamond Platnumz.

Kuleta Ushindani wenye afya kwa lebo kongwe kama WCB, Kings Music na Konde Worldwide.

Ukweli usiofichika ni kuwa suala la wasanii wengi kuanzisha lebo za muziki hutoa changamoto chanya kwa lebo kongwe hapa Tanzania, ambazo aghalab hutawala soko la muziki. Mfano ulio wazi ni mara tu baada ya Rayvanny kumtambulisha msanii wake Mac Voice, mashabiki wengi na vyombo vya habari walianza kumfananisha msanii huyo na wasanii wa lebo nyingine kubwa kama Zuchu wa Wasafi, Ibraah wa Konde gang na hata Tommy Flavor wa Kings Music. Hii inatoa ujumbe kwa lebo kongwe kuwa inatakiwa wawe wabunifu zaidi ili kuendelea kutawala soko la muziki hapa Tanzania.

Kufanya biashara na kuongeza kipato.

Kumiliki lebo ni biashara yenye faida kubwa kwani msanii ambaye anamiliki lebo husika hupata asilimia fulani ya mapato yanayotokana na shows za msanii husika, mirabaha kutoka kwenye mitandao ya kusikiliza muziki au hata mikataba ya ubalozi ya msanii anayemsimamia. Makubaliano hayo baina ya wasanii mara nyingi huwa ni ya siri na huwa inasimama mara tu mkataba unapofikia mwisho.

Leave your comment