Nay Wa Mitego Aeleza Jinsi Usambazaji wa Albamu ya Alikiba Mtaani Umeathiri Mauzo Yake
19 October 2021
[Picha: All Africa]
Mwandishi: Brian Sikulu
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram
Mwanamuziki maarufu kutoka nchini Tanzania Nay Wa Mitego amelalamika kuhusu uuzaji haramu wa albamu ya Alikiba mtaani.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Nay Wa Mitego alieleza kuwa albamu hiyo imefurika mtaani na watu wanayoisambaza wanaathiri vibaya kipato ambacho Alikiba angepata kutokana na mauzo ya albamu hiyo.
Soma Pia: Producer Yogo Beats Asikitishwa Kuona Albamu ya Alikiba Ikiuzwa Mtaani
Alisema kuwa iwapo wachuuzi hao wangeshiriki katika kununua albamu hiyo na kuiuza kwa njia isiyo ya haramu basi msanii husika angefaidika sana.
"The way albam ya officialalikiba ilivyosambaa mtaani endapo hawa wote wangekua wameinunua kwa njia yoyote ile basi mauzo ya hii album yangekuwa ni makubwa sana," ujumbe wa Nay Wa Mitego mtandaoni ulisomeka.
Alikiba aliachia albamu yake rasmi mnamo tarehe saba mwezi huu. Albamu hiyo imepata mafanikio makubwa na imepokelewa vyema ila suala la uuzaji haramu umekithiri na kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau mbali mbali kwenye tasnia ya muziki Tanzania.
Producer Yogo Beats ambaye ndiye alisimamia utengenezaji wa albamu hiyo pia amekwazika na jinsi uuzaji haramu wa albamu hiyo umeongezeka.
Hapo awali, baraza la KOSOTA lilitoa onyo kwa wachuuzi wanouza albamu hiyo mtaani. Kwa mujibu wa taarifa kutoka KOSOTA, yeyote atakayepatikana na kosa la kuuza albamu ya Alikiba kwa njia haramu atapigwa faini ya shilingi milioni ishirini au kutumikia kifungo cha miaka mitano au kuadhibiwa vyote kwa pamoja.
Leave your comment