Diamond Platnumz Atuzwa Msanii Bora wa Afrika

[Picha: Diamond Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki nguli kutokea lebo ya WCB Diamond Platnumz ameshinda tuzo ya msanii bora wa Afrika, kwenye tuzo za Ghana Music Awards ambazo hufanyika huko nchini Uingereza kila mwaka.

Diamond Platnumz ambaye kwa sasa anatamba na ngoma yake ya ‘Naanzaje’ alishinda tuzo hiyo baada ya kuwabwaga wasanii wakubwa waliokuwa wakiwania tuzo hiyo kama Burna Boy, Davido, Wizkid, Master KG, Fireboy DML, Patoranking, Mercy Chinwo, Jude Kay, Sinachi pamoja na Teni.

Soma Pia: Sababu Nne Kuu Zinazowafanya Wasanii Wengi Tanzania Kuanzisha Lebo za Muziki

Ghana Music Awards ni tuzo ambazo hulenga kuwaheshimisha wasanii kutokea nchini Ghana, japo zinafanyika huko nchini Uingereza. Hafla za mwaka huu zimefanyika kwa awamu ya tano kwenye ukumbi wa Royal Regency huko jijini London.

Diamond Platnumz alikuwa ni mwana Afrika Mashariki pekee kwenye kipengele hicho na ushindi wake umepokelewa kwa bashasha kubwa na mashabiki wa muziki. Kupitia ukurasa wa Instagram, lebo ya WCB waliandika wakishukuru waandaaji wa tuzo hizo kwa ushindi huo mnono.

Mwaka 2021 umekuwa ni mwaka wa baraka sana kwa msanii Diamond Platnumz kwani kando na ushindi huu wa sasa, mwezi wa sita alitajwa kuwania kwenye tuzo za BET za huko nchini Marekani japo alipoteza kwa Burna Boy.

Soma Pia: Nyimbo Mpya: Alikiba ‘Oya Oya’, Mac Voice ‘Tamu’ na Ngoma Zingine Zinazotamba Bongo Wiki Hii

Kwa sasa, macho na masikio ya watanzania yameelekezwa kwenye tuzo za AFRIMA ambazo Diamond Platnumz ametajwa kuwania kwenye vipengele tofauti tofauti kama msanii bora wa mwaka, msanii bora wa Afrika Mashariki, wimbo bora wa ushirikiano, mtumbuizaji bora wa mwaka, pamoja na wimbo bora wa mwaka kupitia ngoma yake ya ‘Waah’ aliyomshirikisha Koffi Olomide kutokea Congo.

Leave your comment