Mbinu Alizotumia Diamond Platnumz Kufikisha Watazamaji Bilioni 1.5 Kwenye YouTube

[Picha: Grammys]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Kiwanda cha muziki nchini Tanzania siku tatu zilizopita kililipuka kwa furaha baada ya msanii Diamond Platnumz kuweka rekodi ya kufikisha watazamaji Bilioni Moja nukta tano kwenye mtandao wa YouTube.

Soma Pia: Diamond Aweka Rekodi Mpya YouTube Baada ya Kupata Watazamaji Bilioni Moja Nukta Tano

Kwenye nchi ambayo takriban 40% pekee ya wananchi ndio wana uwezo wa kupata huduma za intaneti, Diamond Platnumz bado ameweka heshima ya chaneli yake ya YouTube kutazamwa sana kuliko chaneli ya mwanamuziki yeyote barani Afrika chini ya jangwa la Sahara.

Swali la kujiuliza ni aliwezaje? Makala hii inaangazia namna ambavyo bosi huyo wa lebo ya WCB amefikisha kiasi hicho cha watazamaji

 Kuchapisha Maudhui ya Aina Tofauti

Kando na kuchapisha video za muziki akaunti ya Diamond Platnumz imesheheni video za matamasha ya Diamond Platnumz, mahojiano yake na vyombo vya habari, maisha yake binafsi na hata video za wasanii wengine mathalan video ya Tanasha Donna ‘Gere’ inapatikana kwenye chaneli ya msanii huyo. Hii imechangia kwa kiasi kikubwa watu kuvutiwa kutembelea chaneli yake.

Soma Pia: Zuchu Aeleza Mbona Diamond Hakuhudhuria Tamasha la Zuchu Homecoming

Uchaguzi Mzuri wa Wasanii wa Kufanya nao Collabo

 Diamond Platnumz mara nyingi kwenye nyimbo zake hushirikisha wasanii wa kimataifa ambao wana ushawishi mkubwa. Mathalan video zilizopata watazamaji wengi zaidi kwenye kwenye chaneli ya msanii huyo ni ‘Yope Remix’, ‘Inama’ pamoja na ‘Waah’ ambazo zote ameshirikisha wasanii wakubwa kutoka Congo. Hii inamaanisha kuwa kushirikisha wasanii kutokea nchi za nje huvuta watu kutoka nchi mbalimbali kuangalia video zake hivyo kuongeza namba ya watazamaji.

Wafuasi Wengi Kwenye Mitandao ya Kijamii

Diamond Platnumz ndiye mwanamuziki anayeongoza kuwa na wafuasi wengi kwenye mtandao wa Instagram Afrika Mashariki akiwa na wafuasi milioni kumi na tatu. Diamond anashikilia namba tatu barani Afrika nyuma ya Davido na Yemi Alade. Hata ukurasa wa Instagram wa lebo yake ya WCB pia una wafuasi milioni tatu nukta tano. Kuwa na wafuasi wengi inarahasisha kazi ya Diamond Platnumz kwani wafuasi hao ndio huenda kuangalia kwa wingi video za msanii huyo huko YouTube pale tu anapotangaza kuwa ameachia video.

Mpangilio Mzuri wa Kutoa Kazi

Diamond Platnumz hafanyi kazi peke yake linapokuja suala la mitandao bali ana timu ya wataalamu wa IT na mitandao ambao hushughulikia YouTube ya msanii huyo. Mmoja ya watu hao ni Kim Kyando ambaye uhusika kupandisha video zote za msanii huyo kwenye chaneli yake ya YouTube na hii imesababisha akaunti ya Diamond platnumz kuwa hai sana kwani video hupandishwa mara kwa mara. Pia, Diamond hana pupa ya kuachia nyimbo nyingi zikifuatana, hivyo wafuasi huwa na hamu kila wakati anapoachia kazi mpya.

Leave your comment