Meja Kunta Aitaja Singeli Kuwa Muziki Bora Zaidi Tanzania

[Picha: Meja Kunta Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Bingwa wa Singeli nchini Tanzania Meja Kunta anaamini kuwa Singeli ndio muziki mkubwa kuliko aina zingine zote nchini humo.

Soma Pia: Meja Kunta Awasihi Wasanii wa Tanzania Hasa wa Singeli Kutumia Kiswahili

Meja Kunta ambaye alitikisa Tanzania na wimbo wake wa ‘Madanga ya Mke Wangu’ miezi michache nyuma kwenye mahojiano katika kipindi cha XXL, ameeleza kuwa kwa sasa muziki wa Singeli ndio umebeba utambulisho wa muziki wa Tanzania.

"Cha kwanza Singeli yani uwezi kupata nchi yoyote yani unapata Tanzania tu na huwezi kufanana na muziki wa aina yoyote. Pia hata vifaa vyake maandalizi yake ni vitu viwili tofauti," alieleza msanii huyo.

Pia Meja Kunta alieleza kuwa muziki huo unafanya vizuri sana nchi za nje kwani aliweza kufanya show nchini India na pia siku chache zijazo anatarajiwa kutumbuiza nchini Uturuki.

Soma Pia: Muziki wa Singeli Tanzania: Kwa Nini Singeli Haitambi Kama Bongo Fleva?

"Nimepata tena show nyingine Uturuki ambayo ntasafiri kesho kutwa mnamo tarehe 29 ntafanya perfomance ….. Si tunaenda kule kupeperusha bendera ya nchi ni kitu kikubwa na tunainspire wasanii wengi," alidokeza msanii huyo.

Kauli hii ya Kunta inaakisi vyema hali halisi kuwa muziki wa Singeli unapiga hatua kimataifa kwani Februari mwaka jana mtayarishaji muziki kutokea nchini Marekani Swizz Beatz kupitia Instagram alionekana kuupenda wimbo wa Meja Kunta ‘Wanga’ alioshirikiana na Lavalava.

Kwa sasa, Meja Kunta ambaye ana wafuasi takriban laki 6 na elfu mbili kwenye akaunti yake ya Instagram anatamba na wimbo wake wa ‘Kidimbwi"’ ambao aliutoa Mei Mwaka huu na mashabiki wameonekana kuukubali sana.

Leave your comment