Nyimbo Mpya: Zuchu Aachia ‘Yalaaaa’

[Picha: News Moto]

Mwandishi: Charles Maganga

Mwanamuziki kutokea lebo ya WCB Zuchu ameachia wimbo mpya kwa jina ‘Yalaaaa’.

‘Yalaaaa’ umeandaliwa na mtayarishaji wa muziki nguli kutokea Tanzania Mocco Genius ambaye pia alihusika kutayarisha wimbo wa Zuchu wa ‘Ashua’ akiwa amemshirikisha Mbosso.

Soma Pia: Video za Diamond, Mbosso, Harmonize na Alikiba Zinazotamba Bongo Wiki Hii

Tofauti na wimbo wake wa ‘Nyumba Ndogo’,  kwenye ‘Yalaaaa’ Zuchu anaonesha upande wa pili wa mapenzi na kwa kutumia sauti yake tulivu. Zuchu anaonesha ambavyo amezama kwenye penzi zito na namna anavyopata furaha pale ambapo mpenzi wake anampagawisha kiasi cha kuomba msaada kutoka ‘serikalini’.

"Naiomba Serikali Kijana apelekwe mbali ananifanya silali siwezi kutafakari," anaimba Zuchu kwenye aya ya pili ya wimbo huu huku kwenye kiitikio akirudia rudia neno  ‘Yalaaaa’ kwa kutumia sauti yake iliyojawa umaridadi.

Wote tunafahamu kuwa Zuchu ametokea visiwani Zanzibar na kwenye ‘Yalaaaa’ Zuchu hajaona hatari kuonesha uzanzibari wake kwani Mocco Genius ametumia ala za muziki wa pwani kama madufu na filimbi kunogesha mdundo wa wimbo huu.

Soma Pia: Sitawaangusha: Zuchu Awashukuru Mashabiki Kwa Kumuunga Mkono

Wimbo huu umeaachiwa zikiwa zimebakia takriban siku nne kabla Zuchu hajaingia uwanja wa Amani huko Zanzibar kwa ajili ya Tamasha lake la Zuchu Homecoming na kibao hiki kinategemewa kurindima sana kwenye tamasha hilo.

Kwa mwaka huu, ‘Yalaaaa’ ni wimbo wa tatu kutoka kwa Zuchu kwani Januari mwaka huu aliachia ‘Sukari’ na mwezi Juni aliachia wimbo wake wa ‘Nyumba Ndogo’  ambao una mahadhi ya Singeli.

Kufikia sasa wimbo huu umeshatazamwa mara elfu thelathini kwenye mtandao wa YouTube.

https://www.youtube.com/watch?v=ZOP4ek_RwOI

Leave your comment