Diamond, Rayvanny, Marioo, Alikiba na Wasanii Wanaotarajiwa Kuachia Wimbo Mpya Wiki Hii

[Picha: Capital News]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Tukiwa tunaelekea ukingoni mwa mwezi Julai bila shaka tuliweza kupata burudani maridhawa kabisa kwa wasanii kama Lavalava, Mbosso, Zuchu, Frida Amani, Harmonize na wengineo wengi. Pamoja na kupata burudani kwa pomoni kuna baadhi ya wasanii kutokea nchini Tanzania wameahidi kutoa kazi zaidi. Makala hii inaangazia wasanii sita ambao wametangaza kutoa kazi mpya hivi karibuni.

Soma Pia: Nyimbo Tano Bora za Amapiano Zilizoachiwa na Wasanii Kutoka Bongo

Marioo

Baada ya wimbo wake wa ‘For You’ kufanya vizuri, Marioo amekuwa kimya kwa muda lakini waswahili wanasema kimya kingi mshindo mkuu na kwa kulitambua hilo, Marioo ametangaza kuachia wimbo mpya uitwao ‘Wow’ ifikapo tarehe 30 Julai mwaka huu. Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Marioo amechapisha video inayoonesha maakuli yakiwa jikoni huku wimbo unaodhaniwa kuwa ndio unaofuata kutoka kwake ukisikika kwa mbali.

Rayvanny

Baada ya EP yake ya Flowers iliyotoka Januari mwaka 2020 kufanya vizuri, hatimaye mkurugenzi mtendaji wa Next Level Music Rayvanny ametangaza ujio wa Flowers II. Rayvany alitoa taarifa kupitia ukurasa wake instagram sehemu ya Instastory ambapo alichapisha picha yenye ujumbe "Flowers II coming soon" akimaanisha watu wakae mkao wa kula kwa ajili ya EP hiyo.

Soma Pia: Nyimbo Mpya: Video Tano 5 Zinazotamba YouTube Tanzania Wiki Hii

Diamond Platnumz

Msanii Diamond Platnumz hajawahi kuishiwa kazi kwenye kapu lake la burudani kwani tayari ameshatangaza kuwa video ya wimbo wake wa ‘Iyo’ iko tayari na itaachiwa saa nne asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki .

Fid Q

Mshindi wa tuzo ya Kili kama msanii bora wa Hip-hop kwa mwaka 2014 Fid Q ameonesha dalili za kutoa wimbo mwezi Agosti mwaka huu. Kupitia account yake ya Instagram Fid Q alichapisha video akiwa studio anarap kisha akasindikiza na ujumbe usomekao "Agosti hii mnataka la kutikisa vichwa (goma moja lenye hisia kali) au la kuchezesha maungo (Banger) au mnataka mnataka yote?

Alikiba

Kutokea King's music msanii Alikiba ametangaza kuwa ndani ya wiki hii ataachia video ya wimbo wake wa ‘Jealous’ aliomshirikisha Mayorkun kutokea nchini Nigeria. Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Alikiba aliandika "Jealous video this week. Inshaallah".

AT

Baada ya wimbo wa ‘Si saizi yao’ aliofanya na Anjella kufanya vizuri, msanii AT ameona aendelee kuporomosha burudani zaidi kwa mashabiki zake. Kupitia ukurasa wake wa Instagram amechapisha video ikimuonesha akiwa studio na kuisindikiza na maneno "Nafikiria sana kufanya kazi na ubora kazi mimi na Anjella tulitest mitambo sasa masikio na macho yenu ju ya Next track".

Leave your comment