TANZANIA: BASATA yatoa agizo kwa wasanii, bila kujisajili hakuna tuzo wala show kama hujajisajili..!
16 February 2016

Yamoto Band ni miongoni mwa makundi yanayofanya show nyingi zaidi nchini.
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) latoa taarifa kuwa bila kujisajili kwa wasanii, hawatapata tuzo wala kufanya show.
Hii ni taarifa zaidi kutoka BASATA;
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) linawataka wasanii wote nchini kuhakikisha wamesajiliwa na kuwa na vibali vya Baraza kwani kufanya vinginevyo ni kuvunja sheria ya Bunge namba 23 ya mwaka 1984 iliyolianzisha BASATA
Ambayo inamtaka mtu yoyote anayejihusisha na shughuli za Sanaa kuwa amesajiliwa na kupewa kibali na BASATA.
Aidha, BASATA linawaagiza Wakuzaji Sanaa wote (Mapromota) wanaoendesha matukio ya Sanaa kama vile matamasha, mashindano, maonyesho na utoaji tuzo nchini kuhakikisha wanafanya kazi na Wasanii waliosajiliwa na wana vibali vyaa BASATA na si vinginevyo.
Sambamba na hii, BASATA linawaagiza wamiliki wote wa studio (Production Houses) zinazozalisha kazi za Sanaa kuzisajili mara moja na kuhakikisha zinakuwa na vibali halali vya Baraza la Sanaa la Taifa.
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa sheria hii ya BASATA, Baraza limepewa mamlaka ya kutoa vibali na kuratibu matukio yote ya Sanaa nchini hivyo kuanzia sasa Baraza litaanza udhibiti wa matukio haya ya Sanaa hasa katika kuongeza sharti la kuwataka waandaaji wote wa matukio ya Sanaa kuwataka Wasanii watakaoshiriki matukio yao kuwa wamesajiliwa na kupewa vibali vya BASATA.
BASATA halitavumilia kwa namna yoyote kuona Mkuzaji Sanaa (Promota) akitumia wasanii wasiosajiliwa na kuwa na vibali kutoka BASATA kwani kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi hasa hiyo namba 23 ya mwaka 1984 inayoelekeza usajili na utoaji vibali kwa wadau wote wa Sanaa.
Itakumbukwa kwamba mnamo mwaka 2013 Serikali kupitia Sheria ya Uhuru wa Forodha ilitangaza rasmi kuzirasmisha sekta za muziki na filamu. Sheria hii pia inawataka wasanii wote nchini kusajiliwa na kupewa vibali na BASATA na kinyume chake ni uvunjaji wa sheria.
Hata hivyo, toka kuanza kwa mchakato huo wa urasmishaji sekta ya Sanaa ni wasanii wa muziki wa injili pekee ndiyo wamekuwa wakisajiliwa kwa wingi huku wale wa kizazi kipya na filamu wakisuasua bila kuwepo kwa sababu za msingi.
BASATA limekuwa likichukua hatua kadhaa kurahisisha mfumo wa usajili wa wasanii ambapo kwa sasa msanii anaweza kupata fomu ya usajili kupitia mtandaoni www.basata.go.tz au kwa maafisa wa Utamaduni wa Wilaya na baadaye kujaza fomu na kutakiwa kuziwasilisha BASATA zikiwa zimeambatanishwa na wasifu binafsi (CV) wa Msanii husika.
Aidha, gharama za usajili ni kiasi cha Tsh. 75,000/- pekee ambapo fomu hupatikana kwa Tsh. 5,000/-, usajili Tsh. 30,000/- na kibali cha kila mwaka Tsh. 40,000/-
Kwa upande wa studio na wakuza Sanaa (Mpromota) gharama ni sawa na msaniii isipokuwa tofauti huwa kwenye kibali ambapo wao hulipa kiasi cha Tsh. 200,000/- kwa mwaka.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA TUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza




Leave your comment