Matukio Tano Ya Kimuziki Yanayosubiriwa Zaidi Tanzania 2023
8 February 2023
[Picha: Instagram]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram
Kwenye tasnia ya muziki, kama kuna mwaka ambao mengi makubwa yanatarajiwa kufanyika basi ni mwaka huu wa 2023. Wasanii wengi wameshadokeza ujio wa albamu zao, matamasha mengi ya muziki yanatarajiwa kufanyika huku wasanii kama Diamond Platnumz, Yammi na wengineo wengi wakiwa tayari wameshauanza mwaka huu kwa kasi sana
Kwa Mwaka 2022 Diamond Platnumz alinogesha Bongo Fleva na First Of All, Killy na Cheed walishangaza mashabiki kwa kuondoka Konde Gang na matukio mengi mengi yaliweza kupamba Bongo Fleva. Vipi kwa mwaka 2022 ni matukio gani makubwa yanayotarajiwa kutokea mwaka huu ? Soma mpaka mwisho :
Tuzo Za Muziki Tanzania
Tangu mwaka 2022 ni rasmi sasa, tuzo za muziki Tanzania maarufu kama Tanzania Music Awards zimerudi na mwaka huu tuzo hizo zinatarajiwa kurindima tena. Kwa mwaka jana Ali Kiba aliibuka kidedea kwa kushinda tuzo nyingi zaidi akifuatiwa na Harmonize pamoja na Nandy.
Tuzo hizo zinatarajiwa kufanyika Aprili au Machi mwaka huu na kulingana na maelezo ya Waziri Wa Utamaduni na Sanaa, Mohamed Mchengerwa huenda tuzo hizo zikawa na mvuto zaidi mwaka huu kwani wasanii wa WCB Wasafi wanatarajiwa kushiriki.
Wasafi Kusaini Msanii Mpya
Siku chache zilizopita, Diamond Platnumz alitangaza kwamba amesaini msanii mpya kwenye lebo yake ya WCB Wasafi na tangu hapo mashabiki wamekuwa na shauku ya kumfahamu ni nani hasa amemwaga wino kwenye lebo hiyo kubwa Afrika.
Ikumbukwe kuwa mara ya mwisho WCB Wasafi kutambulisha msanii mpya ilikuwa ni Aprili 2020 pindi walipomtambulisha Zuchu.
Albamu Ya Zuchu
Kwa mwaka 2021 na 2022 Zuchu kwa nyakati tofauti tofauti amekuwa akidokeza kuhusu ujio wa albamu yake ambayo mashabiki wamekuwa wanaisubiri sana.
Akiongea na kipindi cha Refresh miezi kadhaa nyuma, Zuchu alidokeza kuwa kuchelewa kwa albamu yake kunatokana na baadhi ya wasanii aliowashirikisha kwenye albamu hiyo kushindwa kuwasilisha vipande vyao walivyotakiwa kurekodi.
Tuzo Za MTV Africa Kufanyika Tanzania
Mwezi Mei Mwaka 2023, Wizara ya Sanaa na Utamaduni wakishirikiana na waandaaji wa tuzo za MTV Africa walitangaza kwamba kwa mwaka 2023 tuzo za MTV Africa Awards maarufu kama MAMA zitafanyika hapa nchini Tanzania.
Katika kikao hicho ambacho kilimhusisha Kabalo Kangane ambaye ni mwakilishi wa MTV Africa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara Ya Sanaa, Saidi Yakub, wawili hao waliahidi tuzo hizo kubwa Afrika kufanyika Tanzania mwaka huu, ikiwa ni kwa mara ya kwanza tuzo hizo kufanyika hapa nchini.
Ujio Mpya Wa Christina Shusho
Mwishoni mwa mwaka jana Christina Shusho alitangaza kwamba ndani ya mwaka huu ataachia albamu mpya ya kuitwa Hararat ikiwa ni albamu yake ya kwanza ndani ya miaka minne.
Kwenye albamu yake hiyo, Christina Shusho ametajwa kushirikiana na wasanii tofauti tofauti kutoka Kenya, Congo, Rwanda na mataifa mengine hali iliyochagiza wapenda muziki wa Injili kusubiri kwa hamu albamu hiyo.
Leave your comment