Diamond ‘Number one’, Alikiba ‘Aje’, Na Nyimbo Zingine Zilizopeleka Muziki Wa Bongo Fleva Kimataifa

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pakua Nyimbo za Marioo Bila Malipo Kwenye Mdundo

Sasa hivi imekuwa ni kawaida sana kwa wasanii wa Tanzania kushinda tuzo mbalimbali za kimataifa, kufanya matamasha makubwa ya muziki nchi nyingine pamoja na kushirikiana na wasanii wa mataifa mengine. Miaka 15 iliyopita hii ilikuwa kama ndoto maana Bongo Fleva ilikuwa ikirindima kwenye mipaka ya Tanzania pekee na miaka ya hivi karibuni ndipo mambo yameanza kubadilika kwani muziki wetu huu unasafiri sasa na kuelekea nje ya mipaka.

Zifuatazo ni ngoma tano ambazo zimepelekea muziki wa Bongo Fleva kujulikana zaidi kimataifa:

My Number One Remix - Diamond Platnumz ft Davido

Hii ni ngoma ambayo ilitoka mwanzoni mwa mwaka 2014 na kwa mujibu wa Diamond Platnumz, alitanabaisha kuwa alichukua mkopo benki ili aweze kumlipa Davido na kugharamikia video ya ngoma ya Number One Remix ambayo ilifanyika huko Lagos Nigeria chini ya Clarence Peters. Number One Remix ilimuwezesha Diamond Platnumz kupata uteuzi mara 5 kwenye tuzo Afrimma mwaka 2014 ikiwemo Video ya mwaka Afrika. Ngoma hii pia ndio ilifungua milango kwa wasanii wa Tanzania kuanza kupata nafasi ya kuonekana kwenye vituo vikubwa vya muziki Afrika kama Soundcity, Trace na MTV Base.

https://www.youtube.com/watch?v=Cd2bwLcgGGg

Hawajui - Vanessa Mdee

Ngoma hii kwa mara ya kwanza ilioneshwa Desemba 8, 2014 kwenye kituo kikubwa cha muziki barani Afrika cha MTV Base kitu ambacho kilisaidia sana watu wa mataifa mengine kuufahamu wimbo huu. Ngoma ya Hawajui ambayo ilifanyika huko Afrika Kusini iliweza kufanya vizuri sana kiasi cha kumpatia Vanessa Mdee tuzo ya wimbo bora wa African Pop kwenye tuzo za AFRIMA kwa mwaka 2015. Aidha huu ni wimbo ambao ulipelekea wasanii wengi wa kike Tanzania kama Linah Sanga kuanza kufanya video kubwa huko Afrika kusini kwa lengo la kujitangaza zaidi kimataifa.

https://www.youtube.com/watch?v=Tcs2A9gbbl4

Pakua Nyimbo za Nandy Bila Malipo Kwenye Mdundo

Aje - Ali Kiba

Aje ya Ali Kiba tangu kuachiwa kwake mwezi Mei mwaka 2016 imekuwa ni nembo ya muziki wa Bongo Fleva duniani kwani ngoma hii ilipendwa na watu wa mataifa mbalimbali na ndio maana iliweza kushika namba 2 kati ya nyimbo bora Afrika kwenye chati za muziki za kituo cha Trace Urban cha huko Nigeria. Aidha, Aje iliweza kupata ushindi mnono kwenye tuzo za NAFCA yaani Hollywood & African Film Critics za zilizofanyika huko nchini Marekani ambapo Ali Kiba alishinda tuzo ya Msanii bora wa mwaka na Wimbo bora wa mwaka kwa 2016. Ni kupitia Aje ndo Ali Kiba aliweza kushinda kipengele cha msanii bora Afrika kwenye tuzo za MTV EMA kitu ambacho kilizidi kuheshimisha muziki wetu.

https://www.youtube.com/watch?v=ecywDEswXsI

Muziki - Darassa ft Ben Pol

Pengine ndiyo ngoma ya Hip Hop pendwa zaidi kwenye miaka ya karibuni. Ngoma hii iliweza kuhadithia Afrika kuwa Tanzania pia tunafanya Hip Hop kwani watu wengi maarufu ikiwemo Rais wa Rwanda Paul Kagame alionekana akicheza ngoma ya ‘Muziki’ kwenye sherehe moja huko Kigali Ngoma hii iliweza kuweka rekodi mwaka 2016 baada ya kutazamwa Mara Milioni 1 ndani ya wiki mbili ikiwa ni ngoma ya pili ya Hip Hop kufanya hivyo baada ya ‘Zigo Remix’ ya kwake AY na Diamond Platnumz. Aidha Muziki poa ilitambulisha vyema Hiphop ya Tanzania baada ya kushinda Wimbo bora Wa Afrika Mashariki kwenye tuzo za Hipipo za nchini Uganda kwa mwaka 2018.

https://www.youtube.com/watch?v=DWyiC2CBtyI

Tetema - Rayvanny ft Diamond Platnumz

Hakuna nchi Afrika ambayo wimbo huu haukutetema na ndio maana uliweza kupata remix kutoka kwa wasanii tofauti tofauti Afrika na duniani kwa ujumla kama Patoranking, Zlatan, Pitbull na Mohombi huku hivi karibuni Maluma kutokea Columbia pia alifanya remix ya wimbo huo alioupa jina la Mama Tetema. Tetema ni wimbo ulioweka rekodi tofauti tofauti ikiwemo kufikisha watazamaji Milioni 1 ndani ya masaa 17 tu na pia ni kupitia remix ya ngoma hii yaani Mama Tetema Rayvanny aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza Afrika kutumbuiza kwenye tuzo za MTV EMA.

https://www.youtube.com/watch?v=n6pCgzHMJY8

Leave your comment