Bifu Tano Kubwa Kwenye Bongo Fleva Mwaka 2021

[Picha: Bongo5]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Suala la uhasama na migogoro huwa halikosekani sehemu yoyote na hata kwenye kiwanda cha muziki nchini Tanzania, wasanii mbalimbali kwa mwaka 2021 walionekana kuingia kwenye migogoro kutokana na sababu mbalimbali za kimuziki. Makala hii inagusia bifu tano kubwa ambazo zimetokea baina ya wasanii wa Tanzania kwa mwaka huu wa 2021:

Soma Pia: Nyimbo Tano Kutoka Tanzania Zilizozua Utata Mwaka wa 2021

Harmonize na Rayvanny

Mgogoro huu ulilipuka mwezi Aprili baada ya Rayvanny kulalamika kuwa Harmonize alienda kwenye vyombo vya sheria kwa ajili ya kumshtaki kutokana na kuwa na mahusiano na Paula. Vita baina ya wasanii hawa ilizidi kupamba moto baada ya Harmonize kuachia ngoma yake ya ‘Vibaya’ kuongelea suala hilo, kisha Rayvanny alijibu ngoma hiyo ya Harmonize na ‘Nyamaza’ kabla ya Ibraah kumtetea Harmonize na wimbo wake wa ‘Hayakuhusu’.

AliKiba na Shilole

Mgogoro huu uliibuka baada ya mwanamuziki Ali Kiba kusema kwenye chombo kimoja cha habari hapa nchini Tanzania kuwa hakumualika Shilole kwenye sherehe yake ya kusikiliza albamu yake ya ‘Only One King’. Hiki kilimuudhi sana Shilole. Kupitia mahojiano aliyoyafanya na vyombo vya habari, Shilole alionesha dhahiri shahiri ni kwa jinsi gani alikwazika na kauli hiyo ya AliKiba na kusema kuwa bado hawajakaa chini na AliKiba ili kuzungumza.

Soma Pia: Collabo 10 Kali Kutoka Tanzania Zilizofanya Vizuri Zaidi Mwaka 2021

Roma Mkatoliki na Nikki Mbishi

Mgogoro huu uliibuka mwezi Agosti baada ya Nikki Mbishi kukaririwa akisema kuwa rapa Mkatoliki alipata umaarufu zaidi baada ya kutekwa na watu wasiojulikana mwaka 2017 akiwa rapa mwenzake Moni Centrozone. Kauli hii ilisababisha Roma kuandika ujumbe kupitia akaunti ya Instagram kuwa Nikki Mbishi apunguze chuki badala yake ajikite zaidi katika kutengeneza muziki mzuri kwa ajili ya mashabiki zake.

Harmonize na Dully Sykes

Mgogoro huu uliibuka baada ya Dully Sykes kukubali kuwa yupo kwenye mchakato wa kumshtaki Harmonize baada ya Harmonize kuonekana kutumia vionjo vya wimbo wa ‘Bongo Fleva’ wa kwake Dully Sykes kwenye Amapiano yake ya ‘Teacher’, kitu ambacho kulingana na Harmonize kwenye mahojiano aliyofanya na waandishi wa habari alipokuwa akitua Dar Es Salaam kutoka Marekani ameona sio sawa.

Motra The Future na Mex Cortez

Baada ya Motra The Future kuachia ngoma yake ya ‘Weupe’ ambayo kimsingi ilikuwa ni diss track kwa kundi la Kikosi Kazi, siku chache baadae Mex Cortez aliachia ngoma ya ‘Amkia’ ambayo ilikuwa ni maalum kwa ajili ya Motra The Future. Kufuatia ngoma hizi mbili vyombo vya habari nchini Tanzania vimekuwa vikiripoti hasa kuhusu bifu hili ambalo bila shaka limechangamsha uwanja wa Hiphop nchini Tanzania.

Leave your comment