Harmonize Afichua Idadi ya Nyimbo na Wasanii Walioshirikishwa Kwenye ‘High School’ Album

[Picha: Harmonize Instagram]

Mwandishi: Brian Sikulu

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mkurugenzi mkuu wa lebo ya Konde Music Worldwide Harmonize amefichua idadi ya ngoma zilizomo kwenye albamu yake ifuatayo pamoja na wasanii walioshirikishwa.

Albamu ya Harmonize iliyopewa jina la 'High School' imesubiriwa kwa muda sana tangu msanii huyo kutangaza ujio wake mapema mwakani.

Soma Pia: Alikiba Afichua Sababu ya Kuita Albamu Yake ‘Only One King’

Ikumbukwe kuwa hii ndio itakua albamu ya pili kutoka kwake Harmonize baada ya albamu yake ya kwanza kwa jina la 'Afro East' iliyotoka mwaka jana.

Albamu ya High School inatarajiwa kutoka mnamo tarehe tano mwezi Novemba na ina jumla ya nyimbo ishirini. Albamu imewahusisha watayarishaji wa muziki kumi na wawili. Watayarishaji wa muziki waliohusika katika kutengeneza midundo ya nyimbo kwenye albamu hiyo ni pamoja na: B-Boy Beats, Mr Simon, Black, Abbah, Young Keys, Hunter, Daxo Chali, Dj Tittoh, L.A.X, Eyoo Kenny, YP Kezzy na Steve.

Sita kati ya nyimbo ishirini kwenye albamu hiyo ni kolabo ambazo zimewahusisha wasanii kutoka sehemu tofauti za Afrika. Wasanii walioshirikishwa kwenye albamu hiyo ni pamoja na: Sarkodie, Ibraah, Anjella, Busiswa na Sholo Mwamba.

Soma Pia: 20 Percent Amjibu Harmonize Kuhusu Kufanya Collabo

Ngoma ya 'Sandakalawe' ambayo Harmonize alikua tayari ashaachia yaonekana itafanyiwa remix kwani ipo kwenye orodha ya nyimbo kwenye albamu, japo ameshirikishwa msanii Busiswa.

Ikiwa imesalia takriban wiki moja kabla ya albamu hiyo kutoka rasmi, mashabiki wanasubiri kwa hamu sana. Albamu tatu kubwa zilikuwa zimesubiriwa nchini Tanzania kutoka wasanii Alikiba, Harmonize na Diamond. Tayari Alikiba ashatoa yake na sasa ni zamu ya Harmonize kisha baadaye Simba atanguruma.

Leave your comment