Chege Chigunda Atangaza Kujitoa Katika Kusimamia Wasanii Wachanga

[Picha: Word Press]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki nguli kutokea Tanzania Chege Chigunda ameweka wazi msimamo wake kuwa ameachana na shughuli za kusimamia wasanii kama ambavyo alifanya hapo awali.

Chege ambaye kwa sasa anatamba na ngoma yake ya ‘Kushki’ aliyasema hayo kwenye mahojiano na kituo kimoja cha habari ambapo msanii huyo aliweka wazi kuwa ameacha kabisa kusimamia wasanii wachanga kwani wengi wao sio waaminifu.

Soma Pia: Alikiba Apokea Tuzo Mbili Kutoka YouTube

"Hiyo mitikasi ya kusimamia wasanii nimeamua kuachana nayo kwa sababu ya Trust imekuwa sio nzuri kwa wasanii wanaochipukia. Kwa hiyo mi nimeona nikae pembeni nifanye vitu vyangu mimi na kusapoti watu bila kusema namsapoti nani,” alizungumza msanii huyo.

Kauli hiyo kutoka kwa Chege inakuja siku chache baada ya aliyekuwa msanii wake Mac Voice kutambulishwa kama msanii rasmi wa lebo ya Next Level Music ya Rayvanny.

Hapo awali, Mac Voice alikuwa chini ya usimamizi wa Chege na wasanii hao wawili waliweza kutoa ngoma ambazo zilitamba sana hapa Tanzania kama vile ‘Utarudi’, ‘Damu ya Ujana’ pamoja na ‘Mama J’.

Soma Pia: Nay Wa Mitego Atangaza Ujio wa Albamu Yake Mpya

Aidha, kwenye mahojiano yake Chege ametanabaisha kuwa lebo yake ya Unique Voice Music bado ipo japo inamhusu sana yeye na haipo kwa ajili ya kusimamia kazi za wasanii wengine.

"Unique Voice Music UVM yaani hiyo Unique Voice yenyewe ni mimi. Mimi ndo ambaye nina hiyo sauti ya kipeke yangu kwa hiyo, hiyo lebo unayoisema wewe its me. Inasimamia kwangu kwanza mimi ndo namba moja," alizungumza Chege.

Msanii huyo aliongezea kuwa ataendelea kutoa mchango kwa wasanii wengine kwa mtindo mwingine.

Leave your comment