Ibraah Ajibu Madai ya Kununua Watazamaji wa Wimbo wake ‘Jipinde’ Kwenye YouTube

[Picha: Ibraah Twitter]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Msanii kutokea Konde Gang Ibraah kwa mara ya kwanza amejibu watu wanaotuhumu kuwa amenunua watazamaji kwenye wimbo wake mpya ‘Jipinde’.

Ibraah ameweka wazi kuwa yeye ana wafuasi wengi sana Instagram ambao ni milioni moja nukta tatu hivyo sio jambo la kushangaza yeye kupata watazamaji wengi YouTube kwani mashabiki na wafuasi tayari anao.

Soma Pia: Wimbo Mpya wa Ibraah 'Jipinde' Wamuandikishia Rekodi Mpya

"Followers wangu mimi wanazidi hata hao viewers ambao mnawasema so ni kitu ambacho hakimake sense ukiniambia eti anaboosti au anatumia maroboti maroboti ndo nini?" alihoji msanii huyo.

Wimbo wa ‘Jipinde’ hasa video imeweza kufanya vizuri sana kwani ndani ya masaa matatu iliweza kutazamwa mara laki tatu na nusu na kufikia sasa video hiyo imeshatazamwa mara milioni moja nukta tatu chini ya saa ishirini na nne, hivyo kuweka rekodi mpya katika muziki wa Ibraah.

Aidha, Ibraah kwenye mahojiano aliyoyafanya ameweka wazi kuwa albamu ndio kitu kinachofuata baada ya ‘Jipinde’.

Soma Pia: Rich Mavoko Azungumzia Kufanya Kazi na Harmonize

"Mi nategemea baada ya Jipinde ifuate album nimewaahidi muda mrefu mashabiki zangu alafu mi mziki nikikaa nao ndani sana nachoka," alisema msanii huyo.

Wasanii wengine kutokea Konde Gang pia ambao wameahidi kutoa albamu ni pamoja na Anjella, Killy pamoja na mkurugenzi mtendaji wa lebo hiyo Harmonize.

Ibraah ni mojawapo ya wasanii wanaofanya vyema sana nchini Tanzania na tangu atambulishwe Konde Gang mwaka jana tayari ameshatoa EP mbili ambazo ni ‘Steps’ iliyotoka Aprili mwaka Jana na ‘Karata Tatu’ iliyotoka Januari mwaka huu.

Leave your comment