AY Ataka Tuzo za Muziki Zirudi Tanzania
16 August 2021
[Picha: Big Eye]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram
‘Godfather’ wa muziki wa Bongo Fleva msanii AY siku ya leo amefunguka namna ambavyo anasikitika kwa Tanzania kukosa tuzo za muziki. Msanii huyo aliyeanza muziki kwenye kundi SOG mwaka 1996 kupitia mahojiano yake aliyoyafanya kwenye kipindi cha The Switch aliweka wazi suala la kiwanda cha muziki Tanzania kukosa tuzo ni suala la kusikitisha kwani tuzo huleta hamasa baina ya wasanii.
Soma Pia: S2kizzy: ‘Tetema’ ya Rayvanny Ndio Wimbo Ulioniletea Mafanikio Zaidi
AY alieleza kuwa tofauti na kuwa na ushindani YouTube au kwenye mali binafsi kama magari za wasanii, tuzo ina maana kubwa kwa msanii kwani heshima ya kuwa na tuzo hudumu kwa muda mrefu.
"Hakuna kitu cha msingi kama tuzo unajua ukishapewa tuzo ni kizazi na kizazi. Tuzo inaweza kukaa kiasi kwamba hata wajukuu na wajukuu wakajua kuwa babu yao alishawahi kushindaga kitu Fulani,” AY alisema.
Kauli ya AY inaakisi kwa kiasi kikubwa hali ilivyo nchini Tanzania kwani tangu tuzo za muziki za Kilimanjaro Tanzania Music Awards kukoma mwaka 2015, ni miaka sita imeshatimia sasa na tuzo hazijarudi tena hadi leo.
Soma Pia: Diamond Platnumz Athibitisha Kufanya Kazi na P Diddy Kutoka Marekani
AY kwenye mahojiano hayo alidokeza kuwa kukosekana kwa tuzo za muziki hasa kwa nchi kama Tanzania haileti picha nzuri.
"Kukosekana kwa tuzo kiukweli kwa nchi kama Tanzania ambapo Bongo Fleva imekua kubwa sio kitu kizuri, sio picha nzuri kabisa yaani" alizungumza mwanamuziki huyo.
AY ana uzoefu mkubwa sana linapokuja suala la tuzo kwani tangu aanze muziki amepata tuzo kadha wa kadha kama Kilimanjaro Tanzania Music Awards kwa Mwaka 2007 aliposhinda wimbo bora wa Hip-hop na ‘Usijaribu’ huku mwaka 2010 wimbo wake wa ‘Habari Ndio Hiyo’ aliomshirikisha Mwana FA ulishinda kipengele cha wimbo bora wa kushirikiana. Nje ya nchi, AY ameshashinda Tuzo ya Kisima pamoja na Channel O ya Afrika Kusini.
Leave your comment