Nyimbo Mpya: Marioo Aachia ‘Wow’

[Picha: Marioo Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki maarufu kutokea nchini Tanzania Marioo amewachia wimbo wake mpya kwa jina ‘Wow’.

Kwenye ‘Wow’, Marioo ameweza kubadilika na kufanya wimbo wenye mahadhi ya dansi na kuchezeka na bila shaka wimbo huu unategemewa kufanya vizuri sana kwenye sherehe na sehemu tofauti tofauti za kula raha.

Soma Pia: Marioo Atangaza Tarehe ya Kuachia Albamu Yake Mpya

Tofauti kabisa na nyimbo zake nyingine kama ‘Unanionea’, ‘Raha’ au ‘Inatosha’, kwenye ‘Wow’ Marioo anatumia maneno laini kumsifia mwanamke namna ambavyo ameumbika na kupendeza .

Marioo anafungua aya ya kwanza kwa kuimba "Hivi umeumbwa au umeshushwa unanitisha (Wow), Hivi umetumwa ama umeagizwa kunidatisha kiuno kama hakina mfupa mama mwenye bucha kakujazia nyama, nionyeshe alichokupa Mama Baby show dem."

Soma Pia: Amapiano: Mdundo Unaobadilisha Mitindo ya Muziki wa Bongo Fleva

Kwenye kiitikio Marioo anazidi kunogesha wimbo kwa kurudiarudia maneno huku akisindikizwa na mdundo wa nyimbo unaovutia msikilizaji.

‘Wow’ ni kazi ya mtayarishaji muziki nguli hapa nchini Tanzania Kimambo Beats ambaye ameshafanya kazi na wasanii kama Nandy, Shetta, Gigy Money, Benpol, Jux, Maua Sama na Alikiba huku maandalizi ya mwisho ya wimbo huu yakishughulikwa na Mix Killer.

Kwenye mtandao wa YouTube, ‘Wow’ kufikia sasa imeshatazamwa mara 25,000 ndani ya muda mchache tu tangu kuachiwa kwake.

Aidha ‘Wow’ ni wimbo wa pili kutoka kwa Marioo kwa mwaka huu, wa kwanza ukiwa ni ‘For You’ uliotoka Machi 4 mwaka 2021 wimbo ambao uliweza kufanya vizuri kwani ulikuwepo kwenye chati mbalimbali za muziki nchini Tanzania.

https://www.youtube.com/watch?v=Epy9fd9BisU

Leave your comment