K2ga Aelezea Sababu ya Ukimya wa Kings Music

[Picha: K2ga Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki kutokea nchini Tanzania Karim Zuberi almaarufu kama K2ga ameeleza kwanini wasanii kutokea Kings music hawatoi nyimbo mara kwa mara. Akiwa anaongea na wanahabari hivi Karibuni msanii huyo ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wa "Ndombolo" alielezea kuwa ameshazoea kukaa muda mrefu bila kutoa wimbo na anaifahamu mipango ya Kings Music hivyo haoni kitu chochote ajabu.

Soma Pia: Alikiba, Abdukiba, K2ga na Tommy Flavour ‘Ndombolo’: Nyimbo Mpya Tanzania

K2ga alikaririwa akisema "Kwanza nshazoea alafu naelewa kuwa mipango ya management ipoje kwa hiyo haina haja hata kama tukikaa sana lakini tukitoa imo, kwa hiyo naona kawaida tu.”

Sambamba na hilo, K2ga pia alieleza kwanini bosi wa Kings Music msanii Alikiba alitoa nyimbo mbili mfululizo yaani alitoa wimbo wa ‘Ndombolo’ kisha siku chache baadae akaachia wimbo wake na Rude Boy uitwao "Salute".

"Si watu walikuwa wanataka back 2 back ndo tunawaekea sasa. Wiki ijayo mimi (kutoa wimbo) kwa hiyo jiandaeni tu." alisema K2ga.

Soma Pia: Nyimbo Mpya: Alikiba, Rudeboy Waachia Wimbo Mpya 'Salute'

Kauli hiyo ya K2ga imetoa ishara kwamba Kings Music kwa sasa wanabadilisha mfumo wao wa kutoa nyimbo kwani hapo awali walikuwa wakilalamikiwa na mashabiki zao, kuwa label hiyo ilikuwa inakaa muda mrefu bila kutoa wimbo ukilinganisha na washindani wao ambao wamekuwa wakitoa nyimbo nyingi.

Kings Music kwa sasa wanatamba na wimbo wao wa Ndombolo ambao mpaka sasa umeangaliwa takribani mara milioni 2 na laki tisa tangu kuachiwa wiki kadhaa zilizopita.

K2ga kupitia mahojiano hayo na wanahabari pia aliweka bayana kuwa wazo la wimbo wa ‘Ndombolo’ lilikuja kwake na baada ya Alikiba na uongozi wa Kings music kusikiliza wimbo huo wakaona ni vyema waufanye wote.

 "Ndombolo ni wimbo ambao niliufanya ulikuwepo ni wa kwangu na nilitaka niutoe lakini management ikasema hii ni nyimbo bora sana kwa hiyo tujaribu kuimba wote alafu tujue tunafanyaje," alisema mwanamuziki huyo ambaye anatimiza miaka 29 mwaka huu.

Ikumbukwe kuwa Kings Music kwa sasa ina wasanii wanne ambao ni Alikiba, K2ga, Abdu Kiba pamoja na Tommy flavor hii ni baada ya wasanii Killy na Cheed kutimikia Konde Gang mwanzoni mwa mwaka 2020.

Leave your comment