TANZANIA: Taarifa Ya Kuumwa Ya Sam Wa Ukweli Mpaka Kifo Chake

Usiku wa kuamkia Alhamisi hii zilianza kuzagaa taarifa za majonzi za kifo cha msanii wa muziki, Sam Waukweli baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kwa mujibu wa taarifa za awali muimbaji huyo alianza kuugua ghafla akiwa studio na baadaye kukimbizwa hospitali ya Palestina iliyopo Sinza Kinondoni jijini Dar es salaam kwaajili ya matibabu lakini muda mchache alifariki dunia.

Akiongea na Millardayo usiku huo producer Steve Joniso ambaye alikuwa mara ya mwisho na marehumu, alisema wakati yupo studio akiandaa beat kwaajili ya wimbo wa Sam, muimbaji huyo alikuwa akilalamika kuumwa tumbo na baadaye alizidiwa na kukosa nguvu kabisa hali ambayo ilipelekea hata ashindwe kwenda chooni mwenyewe.

“Ikabidi tumpeleke chooni huwezi amini chooni tulimtenga hawezi kukaa kwenyewe, sisi tukaona hii sio kawaida, tukamwambia Sam ngoja tutoe taarifa kwa ndugu zako, yeye anakataa msiwataarifu, hiyo inaenda saa moja usiku, mida ya saa mbili usiku tukaamua kuwapigia simu ndugu zake tukawataarifu mbwana Sam yupo kwenye hali hii lakini amesema tusiwaambie kama mnaona vipi njooeni. Lakini baada muda mchache tukapigiwa simu ya yule ndugu yake, bwanaee nimeongea na mke wake lakini amesema hana nauli kesho atakuja hapo kumuona, hata mimi nitakuja muda huo huo,” alisema producer huyo.

“Tumekaa mpaka saa nne usiku hali yake ikawa mbaya zaidi, akaomba akapumzike, sisi tukamwambia tukupe dawa yeye akaomba apumzike ila kwa kunisaidia ili nisiwasumbue naomba nifunge pempasi, sisi kama vijana wa kiume tukamchukua tukamfunga pempasi, sisi tukarudi studio kuendelea na kazi,” aliongeza.

Kifo Chake

“Tumekaa dakika tano tu tukagongea kwamba Sam anawaita, kwenda kutamuuliza vipi Sam akasema siwezi kupumua vizuri, nasikia kama nashindwa kupumua, sisi kwa upande wetu tukaona hii imekaa vibaya, tulichokifanya ni moja kwa moja kumpeleka hospitali, tukampeleka mahabara ndogo pale Mabibo, kumpeleka pale wakatuambia huyu jamaa anaumwa sana mpelekeni Palestina. Tumefika Palestina tumefanya process zote baadaye tukaambiwa tumpeleke kwenye emergency wakawa wanamuekea vifaa vya kupumulia baadaye kama dakika 10 tukaitwa bwana nani anahusika nikasema mimi nahusika, wakaniambia njoo tukupe majibu, wakiambia nijikaze huyu ndugu yako hatuko naye tena, sikuamini kwa sababu tulikuwa naye muda mchache uliopita na jana yake tulishinda naye,” alifafanua Steve.

Source: bongo5.com

Leave your comment