Zuchu Afungiwa Kufanya Muziki Zanzibar

Image Source: Online 

Writer: Charles Maganga 

Download New Kalenjin DJ Mixes on Mdundo

Mwanamuziki kutokea lebo ya WCB Wasafi, Zuhura Othman Soud maarufu kama Zuchu hivi karibuni ameingia matatani baada ya kufungiwa kufanya shughuli za sanaa kisiwani Zanzibar. 

Zuchu ambaye kwa sasa anatamba na ngoma yake kali ya mapenzi ya kuitwa Zawadi amepatiwa adhabu hiyo na Baraza La Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni la Zanzibar ikiwa ni saa chache tangu msanii huyo aombe radhi kufuatia sakata hilo. 

Zuchu amefungiwa na Baraza la Sanaa, Sensa, Filamu na Utamaduni la Zanzibar kutofanya shughuli za Sanaa kwa muda wa Miezi 6 visiwani Zanzibar adhabu hii imekuja baada ya tukio la Februari 24 mwaka huu Zuchu wakati akitumbuiza katika usiku wa Fullmoon Kendwa Mkoa wa Kaskazini Unguja kudaiwa kuimba nyimbo, kutoa matamshi na kuonyesha ishara mbaya ambazo ni kinyume na maadili ya kizanzibari.

Akizungumza leo Machi 5, 2024 ofisini kwake na waandishi wa habari, katibu mtendaji wa baraza hilo, Omar Abdalla Adam amesema baraza limemfungia kwa kipindi cha miezi sita kuanzia sasa.

"Baraza lina wajibu wa kusimamia mila, silka desturi na utamaduni wa Mzanzibari, kwa hiyo linatamka rasmi kumfungia msanii Zuhura Othman Soud (Zuchu) kufanya shughuli yoyote ya sanaa kwa Zanzibar kwa kipindi cha muda wa miezi sita kuanzia leo Machi 5, 2024," alizungumza katibu wa baraza hilo. 

Kando na Zuchu, wasanii wengine ambao wameshawahi kufungiwa kufanya kazi za sanaa ni pamoja na Gigy Money, Billnass na Rayvanny. 

 

Leave your comment