Orodha washindi Tuzo za FIFA - Argentina wapepea- Mdundo Alt

[Picha: Skysports]

Mwandishi: Stellah Julius

Pata na upakue Ubashiri wa Mechi mbalimbali ndani  ya Mdundo

Usiku wa Februari 27 tuzo za FIFA zilitolewa huko Paris na Argentina wameng'ara zaidi katika tuzo hizo wakiondoka wakiwa wamebeba tuzo zaidi ya nne katika Jiji Hilo la mitindo nchini Ufaransa. Wafuatao ni washindi wa tuzo hizo zinazotolewa na FIFA.

MCHEZAJI BORA WA FIFA WANAUME

Akiwapiga chini Karim Benzema pamoja na Kylian Mbappe, Lionel Messi ameibuka mshindi wa tuzo hiyo ya mchezaji Bora Kwa upande wa wanaume. Hili limekuja  kutokana na mchango wake mkubwa katika timu yake ya Taifa kwa kuifanikisha Kushinda kombe la dunia na kuondoka kama mchezaji Bora katika mashindano hayo yaliyofanyika mwishoni mwaka 2022.

 

MCHEZAJI BORA WA FIFA WANAWAKE

Kwa misimu miwili mfululizo kutokea katika timu ya Barcelona na timu ya Taifa ya Uhispania Alexia Putellas ameibuka mshindi katika kinyang'anyiro hicho cha mchezaji Bora Kwa upande wa wanawake. Katika tuzo hiyo Putellas alikuwa akichuana na Alex Morgan pamoja na Beth Mead.

 

MLINDA MLANGO BORA WA FIFA WANAUME

Kutokea Argentina Emiliano Martinez ndiye mshindi kama golikipa Bora wa FIFA katika mchuano mkali alipokuwa akichuana na Thibaut Courtois wa Real Madrid pamoja na Yassine Bounou aliyeipeleka Morocco mpaka katika nafasi ya tatu kombe la Dunia mwaka 2022.

MLINDA MLANGO BORA WA FIFA WANAWAKE

Akiwa anakipiga huko Manchester United Kwa upande wa wanawake Mary Earps ndiye mshindi huku mashindano ya Euro 2022 yakimfanya kuonekana Moja kati ya wachezaji wazuri uwanjani. Katika kipengele hicho Earps alikuwa akichuana na Ann-Katrin Berger anayekipiga katika timu ya Taifa ya Ujerumani pamoja na Chelsea na mpinzani mwingine akiwa Christiane Endler raia wa Chile anayeitumikia klabu ya Lyon ya Ufaransa

KOCHA BORA FIFA WANAUME

Akiwa Moja kati ya makocha wenye umri mdogo Lionel Scaloni ameshinda katika kinyang'anyiro Cha kocha bora kwa kuwapigia kikumbo Pep Guardiola wa Manchester city pamoja na Sharobaro Mzee bishoo Carlo Ancelotti wa Real Madrid

KOCHA BORA FIFA WANAWAKE

Mwanamama Sarina Wiegman Hana hiyana kubeba pongezi kama kocha bora kwa upande wa wanawake. Huu ndiye Mwalimu katika kikosi Cha Simba jike wa Uingereza Lioness aliyewapatia mbinu za kuondoka na ubingwa wa Euro 2022. Wapinzani wake walikuwa Pia Sundhage na Sonia Bompastor.

KIKOSI BORA CHA FIFA WANAUME

Thibaut Courtois, Achraf Hakimi, Joao Cancelo, Virgil van Dijk, Kevin De Bruyne, Luka Modric, Casemiro, Lionel Messi, Kylian Mbappe, Karim Benzema, Erling Haaland.

Katika orodha ya kikosi Cha wachezaji Bora upande wa wanaume PSG, Manchester City pamoja na Real Madrid imeingiza wachezaji watatu kila timu.

KIKOSI BORA CHA FIFA WANAWAKE

Christiane Endler, Lucy Bronze, Mapi Leon, Leah Williamson, Wendie Renard, Alexia Putellas, Keira Walsh, Lena Oberdorf, Alex Morgan, Sam Kerr, Beth Mead.

Licha kuchukua tuzo ya mlinda mlango Bora lakini Mary Earps katika kikosi Bora Cha FIFA hayupo.

TUZO YA MASHABIKI BORA

Kwa mara nyingine tena Argentina wameziteka tuzo hizi za FIFA baada ya mashabiki wao nao kuwa Moja kati ya watu walioonesha mchango wao katika timu hiyo hata kabla ya ushindi wa kombe la Dunia. Kutinga fainali pekee kuliwapeleka mashabiki nyumba kwa aliyekuwa bibi wa Messi huku wakiimba kwa shangwe.

TUZO YA GOLI BORA - Puskas award

Tuzo hii ya Goli bora imeenda kwa Marcin Oleksy baada ya kufunga kwa mkasi wakati timu yake ya Warta Poznan ilipokuwa ikicheza na Stal Rzeszow.

Tuzo zingine ni pamoja na Fair play award ambayo amepewa Luka Lochoshvill baada ya kuokoa maisha ya mchezaji Georg Teigl kwa kumsaidia kupumua mara baada ya kudondoka wanjani.

Leave your comment