Zuchu Anogesha Msimu Huu Wa Valentine Na "Utaniua"

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram

Msanii nguli kutokea Tanzania Zuhura Othman Soud maarufu kama Zuchu, hivi leo ametimiza ahadi aliyoiweka kwa mashabiki baada ya kuachia ngoma yake iliyosubiriwa kwa hamu ya kuitwa,  Utaniua.

Zuchu alidokeza kuhusu ujio wa ngoma hii ya Utaniua kupitia ukurasa wake wa Instagram siku mbili nyuma pale alipochapisha kionjo cha ngoma hiyo na hivyo kuleta shauku kwa mashabiki zake kuhusu ujio wake huo mpya. Hii ni ngoma ya kwanza kutoka kwa Zuchu kwa mwaka huu wa 2023.

Kwenye Utaniua, Zuchu anatuletea Uzanzibari wake kwani anatumia sauti yake tulivu kusifia mapenzi na jinsi ambavyo mwandani wake anampenda na kumjali. Ndani ya ngoma hii Zuchu anashukuru na kukiri dhahiri shahiri kuwa amezama kwenye penzi zito kiasi cha kuacha funguo za raha zake kwenye mfuko wa mpenzi wake.

Aidha, kwenye Utaniua  Zuchu ametumia mtindo wa Bongo Fleva huku akiremba ngoma hii na Kiswahili sanifu pamoja na mashahiri mepesi ya mapenzi. Bila shaka ngoma hii inatukumbusha Zuchu yule wa 2020 ambaye alitetemesha Afrika Mashariki na EP yake ya "I Am Zuchu"

Ngoma hii imetayarishwa na Trone, mtayarishaji wa muziki kutoka Tanzania ambaye pia alishirikiana na Zuchu katika kutayarisha ngoma ya Sukari ya mwaka 2021, ambayo ilikuwa ndio ngoma iliyotazamwa zaidi kwenye mtandao wa Youtube kwa mwaka 2021 kusini mwa jangwa la Sahara.

https://www.youtube.com/watch?v=e3erBs1myQo

Leave your comment