Bongo Flava Halisi: Mashabiki Wafurahia Ujio Mpya Wa Diamond Platnumz
6 February 2023
[Picha: Instagram]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram
Tangu mwaka 2023 uanze Diamond amekuja kwa kasi kubwa. Ndio kwanza ni mwezi Februari lakini tayari ameshaachia ngoma tatu na mbili kati ya hizo yaani Yatapita pamoja na Zuwena zimeonekana kukosha sana mashabiki wa muziki ndani na nje ya nchi.
Kwenye mitandao ya kijamii kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu ngoma hizo huku wengi wakionekana kusifia na kumvika mataji mengi Diamond. Hata kwenye mtandao wa Youtube namba za Diamond Platnumz zimekuwa kubwa mno ambapo ngoma yake ya Yatapita tayari imeshakusanya views Milioni 7 huku Zuwena ikikusanya view takriban Milioni 3 ndani ya siku tatu tu kitu ambacho ni nadra sana kutokea.
Zifuatazo ni baadhi ya sababu zilizochagiza Zuwena na Yatapita kupokelewa vizuri sana na mashabiki.
Kurudi Kwenye Bongo Fleva
Kwa muda mrefu sasa mashabiki wamekuwa wakilalamika kuwa Diamond Platnumz amekuwa akitembelea sana Afrobeats Na Amapiano na kuisahau Bongo Fleva, kitu ambacho kinathibitishwa na ngoma zake kama Gidi, Sona, Wonder, Iyo na nyinginezo nyingi.
Diamond Platnumz kuachia Zuwena na Yatapita ni kuwakumbusha mashabiki zake Diamond wa kipindi kile cha Kamwambie, Mbagala, Nitarejea na hata Mawazo. Hii imepelekea ngoma hizi mbili kuwa na mwitikio mkubwa sana.
Namna Ya Kutoa Ngoma
Mashabiki walikuwa wanamtamani Diamond Platnumz yule ambaye alikuwa anatoa ngoma kwa mpigo kama ambavyo alifanya mwaka 2014 alipotoa Mdogo Mdogo na Bum Bum kwa pamoja.
Diamond Platnumz kutoa ngoma tatu ndani ya muda mfupi kumeamsha hari ya mashabiki na kuona kuwa njaa, kiu na mzuka wa Diamond Platnumz yule wa 2014 umerudi tena.
Video Kali
Ili kutayarisha Yatapita na Zuwena, Diamond Platnumz aliamua kushirikiana na Director Ivan kutuletea video ambazo watanzania walikuwa wanazihitaji sana, yaani video ambazo zina stori nzuri ambazo wengi wataweza kuendana nazo.
Kwenye Yatapita, Diamond Platnumz alituonesha maisha ya uswahilini kuanzia kero za kwenye Daladala, ubovu wa nyumba za kupanga na mengineyo mengi. Kwenye Zuwena Diamond Platnumz aliakisi vyema maisha ya vijijini na changamoto zake.
Vitu hivi vimegusa sana maisha ya wengi ambao wanaishi au washawahi pitia kwenye maisha kama hayo.
Utunzi Mzuri
Wote tunafahamu ufundi wa Diamond Platnumz katika kuandika nyimbo lakini kwa kipindi cha hivi karibuni Simba ni kama aliuficha kwa muda ufundi huo na kujikita zaidi kwenye midundo ya Amapiano na Afrobeats.
Ukisikiliza vizuri Yatapita na Zuwena hizi ni ngoma ambazo zinahadithia mengi kuhusu maisha ya kila siku ambayo watu wanapitia. Tamathali za semi zimezingatiwa, kiswahili sanifu na kwenye ngoma hizi mbili Diamond hajajaribu hata chembe kuweka pijini ya Nigeria.
Hiki ni kitu ambacho kimechagiza wengi kupenda ngoma hizi mbili hivyo kufanya vizuri zaidi.
Maudhui Safi
Diamond Platnumz alipotoa ngoma kama Kamata na Gidi baadhi walilalamika kuhusu maudhui na mashahiri yalikuwa ni ya kikubwa.
Lakini kwenye Yatapita na Zuwena Diamond Platnumz kwa makusudi kabisa anakwepa rungu la BASATA kwa kutumia lugha safi isiyo na utata ambayo unaweza ukasikiliza na yoyote bila kujali umri au muktadha. Hii pia imechagiza watu wengi kupenda sana ngoma hizi mbili.
Leave your comment