Wasanii Watano Wa Kutazama Zaidi Bongo 2023

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram

Mwaka 2022 tuliona mengi sana kwenye tasnia ya muziki Tanzania, ikiwemo Diamond Platnumz kufikisha watazamaji Bilioni 2 Youtube, Zuchu kushinda Afrimma, Marioo kuachia albamu yake ya The Kid You Know na mengi sana ambayo wasanii wa kiwanda hiki cha Bongo Fleva walituletea.

Kwa mwaka huu mambo mengi mazuri zaidi yanatarajiwa kufanyika na kuna baadhi ya wasanii ambao ukiwaangalia kwa jicho la tatu wanaweza kufanya makubwa zaidi. Hawa ni wasanii 5 kutoka Tanzania ambao wanatazamiwa kuleta mabadiliko na kufanya vizuri zaidi kwa mwaka 2023.

Vanillah Music

Mara baada ya kutambulishwa kama msanii wa Kings Music mwishoni mwa mwaka jana Vanillah alituburudisha na EP yake ya kuitwa Listen To Me ambayo ilimtambulisha vyema. Kwa mwaka 2023 bila shaka Vanillah ataendelea kuimarisha nafasi yake kwenye Bongo Fleva.

Wengi wanasubiri kuona collabo yake na Ali Kiba na pengine tunaweza tukamuona Vanillah mpya ambaye anaweza akajaribu kufanya mitindo mipya ya muziki kama Amapiano, Afrobeats.

https://www.youtube.com/watch?v=TcT_rGQsyN4

Zuchu

Bila shaka Zuchu ana mengi ya kujivunia kwa mwaka 2022 kwani aliweza kushinda tuzo ya AFRIMMA na kuweka rekodi ya kuwa msanii wa kike chini ya jangwa la Sahara, kuwa na subscribers (wafuatiliaji) wengi Youtube.

Kama alivyotuahidi, kubwa linalosubiriwa kwa Zuchu kwa mwaka huu wa 2023 ni albamu yake ambayo amekuwa akiidokeza kwa muda mrefu sana sasa. Kuhusu albamu hiyo Zuchu alidokeza kuwa amekuwa akiiandaa kwa muda mrefu na kwamba kinachochelewesha albamu hiyo ni kutokana na baadhi ya wasanii aliowashirikisha kuchelewa kurekodi vipande vyao vya nyimbo

 

Kontawa

Mwaka 2022 ulikuwa mzuri sana kwa Kontawa kwani kupitia ngoma yake ya Champion, Kontawa alijulikana na Tanzania nzima na kuweza kufanya kazi na wasanii tofauti tofauti ikiwemo Harmonize.

Kwa 2023, mashabiki wana hamu ya kufahamu je Kontawa ataleta nini kipya. Kama atatoa EP, albamu au kufanya collabo na msanii mwingine mkubwa, Kontawa, bila shaka anatarajiwa kufanya vizuri 2023.

Aslay

Aslay amerudi na ngoma zake mbili yaani Moza pamoja na Follow Me ambayo amemshirikisha Harmonize na kwa mwaka 2023 mambo yanatarajiwa kuwa sukari zaidi kwa Aslay ambaye kwa sasa yuko chini ya lebo ya Rockstar Africa.

Baada ya kusainiwa Sony Music, Je Aslay ataendelea kutoa ngoma za Bongo Fleva kwa ajili ya Afrika Mashariki au atajaribu kupenya katika masoko mengine tofauti tofauti kama Nigeria, Afrika Kusini na nchi nyingine.

 

Phina

Phina aliweza kujihakikishia nafasi yake  kwenye Bongo Fleva kupitia ngoma yake ya Upo Nyonyo na ushindi wake kama msanii bora chipukizi kwenye tuzo za Tanzania Music Awards. Wengi wanasubiri kumuona Phina mpya ambaye ataendeleza alichokianzisha 2022.

Mashabiki wengi wanasubiri kusikia EP au albamu kutoka kwa Phina kwa mwaka huu wa 2023.

 

Leave your comment