Anjella Afunguka Kwa Mara Ya Kwanza Baada Ya Kuondoka Konde Gang

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram

Msanii mwenye kipaji cha aina kutokea Tanzania, Anjella, hivi karibuni amepamba kurasa na vichwa vya habari mbalimbali nchini baada ya kuzungumza kwa mara ya kwanza baada ya tetesi za muda mrefu kuwa ameshaondoka kwenye lebo ya Konde Music Worldwide ya kwake Harmonize.

Katika nyakati tofauti tofauti Harmonize alitangaza kwamba Anjella tayari ameshaondoka Konde Gang ambapo kupitia  Champion Remix, Harmonize aliweka wazi kuwa kwa sasa Konde Gang amebaki yeye na Ibraah. Aidha hivi karibuni Anjellah alionekana akiwa kwenye makao makuu ya Baraza La Sanaa La Taifa BASATA, kitu ambacho kiliashiria kuwa hitmaker huyo wa Nobody yuko kwenye hatua za mwisho za kuondoka Konde Gang.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Anjella hivi karibuni aliaga na kutangaza rasmi kuondoka Konde Gang na kupitia mahojiano aliyoyafanya na Clouds E ya Clouds TV Anjellah alidokeza kwa mara ya kwanza kwamba ni kweli ameshaondoka Konde Gang na kwamba mashabiki wake wawe na subira

" Mi nadhani kila kitu nitakuja kuwaambia lakini natamani mashabiki zangu wawe na subira yaani sijui nisemeje lakini kila kitu nitakuja kukiweka wazi. Kwa hiyo watu tu wawe na subira." alizungumza msanii huyo ambaye hivi karibuni alitajwa kuwania kama  msanii bora chipukizi kwenye tuzo za AEAUSA.

Ikumbukwe kuwa Anjella alijiunga Konde Gang mwaka 2021 baada ya Harmonize kuweza kuona uwezo wake wa kuimba kupitia Instagram na tangu kusainiwa Konde Gang Anjella ametoa ngoma nyingi kali kama Kioo pamoja na Nobody.

Leave your comment