Ufaransa Yaibua Hisia Mseto Baada Ya Kushindwa Kwenye Kombe La Dunia

[Picha:Instagram]

Mwandishi: Stellah Julius

Pata na upakue Ubashiri wa Mechi mbalimbali ndani  ya Mdundo

Fainali za kombe la dunia nchini Qatar zimemalizika siku ya Decemba 18 mara baada ya Argentina kuwatoa machozi Ufaransa kwa mikwaju ya Penalti.

Ufaransa waliokuwa mabingwa watetezi walishindwa kutetea kombe hilo la dunia mbele ya Rais wao Emmanuel Macron aliyehudhuria fainali hizo zilizofanyika katika uwanja wa Lusail na kuhudhuriwa na zaidi ya watazamaji 88000.

Pigo hili kwa Ufaransa linamrudisha kocha wa timu hiyo Didier Deschamps na majonzi nchini Ufaransa baada ya kushindwa kutetea nafasi yao ya kombe la dunia baada ya kufungwa mikwaju ya Penalti 4-2.

Fainali hizi za kombe la dunia kwa Ufaransa ni jumla ya mechi 2 walizoambulia kichapo baada ya mechi yao ya makundi waliyofungwa na Tunisia bao 1 kwa sifuri.

Hizi ni fainali za aina yake kutokana na upinzani uliojitokeza kwa pande zote mbili na hatimaye mchezo kumalizika kwa uamuzi wa penalti. Mastaa mbalimbali dunia kote walishindwa kujizuia na kutumia mitandao yao ya kijamii kueleza hisia na uoga waliokuwa nao juu ya fainali hizo.

Mmoja wao ni nyota wa tenesi kutokea nchini Marekani Serena Williams aliyetweet ya kuwa `sawa kama nitapata mshituko wa moyo ni kwa sababu naangalia kombe la dunia '

Baada ya matokeo hayo mshindi wa kombe la dunia mwaka 2018 Paul Pogba naye aliwatia moyo Ufaransa kupitia ukurasa wake wa Instagram kwa Kuandika `Ndani na nje ya uwanja bado nitakuwa nanyi' .

Pia naye Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika ya kuwa 'Hongera timu ya Ufaransa kwa kazi yake na upambanaji wake katika Kombe hili la Dunia. Umelifurahisha Taifa na wafuasi duniani kote. Hongera Argentina kwa ushindi wao.

Naye pia Mkurugenzi wa Twitter Elon Musk kupitia ukurasa wake wa Twitter aliandika ya kuwa baada ya Ufaransa kufungwa tweet 24,400 ziliandikwa kwa sekunde na kusema ni tweet nyingi kuwahi kutokea Katika michuano ya kombe la dunia.

Zaidi ya dakika 70 za mchezo Ufaransa walionesha kuzidiwa lakini baada ya Mbappe kushinda penalti katika dakika ya 80 Ufaransa walirudi mchezoni na kuonesha upinzani wa hali ya juu kwa Argentina.

Hatimaje Argentina wameondoka na kombe la tatu la dunia na Ufaransa kumaliza katika nafasi ya pili baada ya kushindwa kutetea nafasi yao hiyo.

 

Leave your comment

Top stories