Harmonize "Made For Us" Jux, King of Hearts' na Albamu Zingine Bora Zilizoachiwa mwaka 2022 Tanzania
14 December 2022
[Picha: Instagram]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram
Mwaka 2022 huko ukingoni na upande wa kiwanda cha muziki nchini Tanzania itoshe kusema soko la albamu liliweza kutaradadi sana kwani wasanii wengi waliweza kutuburudisha, kutupa mawaidha kuhusu maisha na kutufungulia tusiyoyajua kuhusu maisha yao kupitia albamu za muziki walizoziachia.
Huu ni mwaka ambao Harmonize alitikisa na Made For Us, MansuLi alituhadithia hadithi nzuri za mapenzi kwenye Love Life, Marioo alitujuza kuhusu maisha yake kwenye "The Kid You Know" na wasanii wengine waliachia albamu ambazo ziliweza kutengeneza historia ya aina yake kwenye muziki wa Tanzania.
Zifuatazo ni albamu bora na ambazo zilifanya vizuri zaidi Tanzania kwa mwaka 2022:
Made For Us - Harmonize
Made For Us ni moja kati ya albamu bora kuwahi kutokea kwenye kiwanda cha muziki Tanzania. Kupitia ngoma kama "Leave Me Alone," Nitaubeba", "You" na "Mwenyewe" Harmonize aliidhihirishia dunia kwamba ana uwezo mkubwa wa kuandika ngoma na kutunga mashahiri ambayo yatasuuza hisia za mashabiki.
Pamoja na kutofanya promotion kubwa kama ambavyo imezoeleka lakini melodies kali, uandishi wa aina yake pamoja na hadithi nzuri kutoka kwa Harmonize zimechagiza ‘Made For Us’ kuwa moja kati ya albamu bora kwa mwaka 2021.
The Kid You Know - Marioo
Kama unataka kumfahamu Marioo kwa undani basi unaweza kuokota mengi sana kupitia "The Kid You Know" albamu yenye ngoma 17 ambazo ndani yake Marioo anaranda randa kwenye aina tofauti tofauti za muziki kama Amapiano, R&B, Afro Beats pamoja na Bongo Fleva.
Kupitia ngoma kama "I Miss" akiwa na Ali Kiba pamoja na "Lonely" ambayo kafanya na Loui, bila shaka Marioo ametumia albamu hii ya "The Kid You Know" kuonesha kwamba anaweza kufanya aina tofauti tofauti za muziki na bado akaendelea kutoa hits.
King Of New School - Ibraah
Ibraah wa Konde Gang nae alipamba mwaka 2022 na albamu yake ya "King Of New School" ambayo ndani yake aliongelea mapenzi pamoja na maisha kwa ujumla huku akiwa amepata usaidizi wa aina yake kutoka kwa Maudi Elka, Christian Bella, Waje, Roberto na wengineo wengi.
Love Sounds Different - Barnaba Classic
Ili kuadhimisha miaka yake 18 ndani ya muziki huu wa Bongo Fleva, Barnaba hakuona hatari kumchukua Diamond Platnumz, Ali Kiba, Rayvanny, Marioo, Lody Music, Nandy na wengineo wengi ili kutengeneza albamu ambayo kwa mwaka 2022 imeweza kuteletea mikwaju mikali kama "Hadithi", "Marry Me", "Mzuri" pamoja na "Tamu".
Goddess - Rosa Ree
Ukisikiliza albamu ya Goddess ya Rosa Ree utapata hisia mseto ambapo unaweza kujikuta unapata hamasa, raha, hasira, wasiwasi lakini kubwa kabisa kuridhika na maisha. Goddess ni albamu ya kwanza ya Rosa ree tangu aanze muziki na humo ndani ameshirikisha wasanii tofauti tofauti kama A Pass, Christian Bella, Nadia Mukami, Fid Q, Cherry na wengineo wengi.
Msodoki Super Nyota - Msodoki Young Killer
Ili kukamilisha albamu hii ya Msodoki Super Nyota Young Killer aliamua kushirikisha wasanii kama Nikki Mbishi, Country Wizzy, Maarifa pamoja na Mr Blue. Hii ni moja kati ya albamu bora za Hip hop kutoka Tanzania kwa mwaka 2022 ambapo Young Killer amezungumzia kuhusu kazi yake ya muziki, ushindani uliopo, kutopenda kushindanishwa na wasanii wengine na mambo mengine mengi.
King Of Hearts - Jux
Hii ni moja kati ya albamu ambazo zilisubiriwa kwa hamu sana na mashabiki wa muziki Tanzania kwa mwaka 2022.
Ngoma zilizomo kwenye albamu hii kama "Nidhibiti" ambayo kamshirikisha Zuchu pamoja na "Lucky Now" akiwa na Bien bila shaka sio tu kwamba zimeonesha kwamba Jux ana kipaji kikubwa cha uandishi lakini pia zimeonesha ukuaji na uwezo wa Jux kufanya aina tofauti tofauti za muziki.
Dedication - Ommy Dimpoz
Ommy Dimpoz hakuwa anatania aliposema kwamba "Dedication" ndiyo albamu bora ya mwaka, kauli ambayo inathibitishwa na ngoma kama "I got You", "Marry You" pamoja na "My Queen".
Kwa Ommy Dimpoz ambaye ana miaka zaidi ya kumi kwenye tasnia ya Bongo Fleva bila shaka Dedication imekuwa ni project ambayo iimemleta Ommy Dimpoz mpya ambaye hata wasanii wa kizazi kipya wanatakiwa wajifunze kutokea kwake.
Rais Wa Kitaa - Nay Wa Mitego
Kwa Nay Wa Mitego, kuwasemea wananchi ndio kipaumbele chake cha kwanza kwenye muziki na ndio maana albamu yake ya Rais Wa Kitaa imebeba hadithi mbalimbali za kusisimua ambazo moja kwa moja zinagusa maisha ya wengi.
Kufanikisha "jambo lake" Nay Wa Mitego alikuwa muungwana na kuomba usaidizi kutoka kwa wasanii kama Ali Kiba, Marioo, Maua Sama pamoja na Runtown kutoka huko nchini Nigeria.
Love Life - MansuLi
Albamu ya Love Life ya MansuLi inaweza isiwe albamu pendwa kwa mashabiki wa kizazi kipya lakini kwa waasisi wengi wa Bongo Hip Hop, albamu hiyo ni kama zawadi kwao.
Kuanzia mpangilio wa ngoma za kwenye albamu, michano mikali ya MansuLi lakini kubwa zaidi ufundi wa MansuLi katika kuhadithia hadithi za mapenzi ndio vitu vilivyochagiza albamu hiyo iwe ya kipekee sana.
Leave your comment