Aslay Atangaza Rasmi Kujiunga Na Lebo Ya Rockstar

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pakua Ngoma Zake Mac Voice Bila Malipo Kwenye Mdundo

Baada ya ukimya wa muda mrefu hatimaye mwanamuziki kutoka nchini Tanzania, Aslay amefunguka hivi karibuni kuwa amejiunga na lebo kubwa hapa Afrika Mashariki ya kuitwa Rockstar ambayo ipo chini ya Christine Mosha maarufu kama Seven.

Aslay ametoa taarifa hizo hivi karibuni ikiwa ni takriban mwaka mmoja na miezi 7 tangu aachie ngoma yake ya mwisho ya kuitwa "Nashangaa" ambayo aliiachia mwaka 2021 huku miezi kadhaa aliachia ngoma ya kuitwa "Mama" ambayo ilikuwa ni maalum kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Kupitia akaunti yake ya Instagram Aslay ambaye alikuwa pia ni mmoja ya wanamuziki waliounda kundi la Yamoto Band alitangaza kuwa amejiunga na lebo ya Rockstar na kuwaaminisha mashabiki zake kuwa wasubiri mengi makubwa na, mazuri kutoka kwake kwenye safari yake hiyo mpya na Rockstar, lebo ambayo pia ilikuwa inasimamia kazi za Ali Kiba miaka ya nyuma.

"Ninafuraha kuwaambia Mashabiki, Vyombo vya habari na kila anayenifuatilia kwamba hivi karibuni nimejiunga na RockStar Africa @rockstarafrica. Imekuwa safari ndefu yenye matumaini makubwa katika kusimamia kazi zangu za muziki. Hivyo basi, Nawaarifu kutegemea mengi makubwa katika muziki wangu na kuniona katika hatua kubwa zaidi.

Nina kila sababu ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kipindi chote ambacho nilikuwa kimya, hakika nimejifunza Mengi. Ningependa kuchukua wakati huu pia kutoa shukrani zangu kwa kila mmoja wenu kwa support mnayoendelea kunipa katika muziki wangu hata wakati nilipokuwa kimya. Asanteni sana" aliandika Aslay kwenye ukurasa wake Instagram.

Aslay anakuwa ni msanii wa nne ambaye amesainiwa na lebo ya Rockstar kwa sasa, wasanii wengine ambao wako Rockstar ni pamoja na Ommy Dimpoz, Abigail Chams pamoja na Young Lunya.

https://www.youtube.com/watch?v=ciCJ2E1Qg1U

Leave your comment