Nandy Apokea Cheti Cha Grammy

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Kwenye Telegram

Mwanamuziki kutokea nchini Tanzania  Faustina Charles Mfinanga maarufu kama Nandy ameandika historia ya aina yake kwenye muziki wa Bongo Fleva baada ya kupata cheti kutoka kwa waandaaji wa tuzo kubwa za Grammy.

Nandy ambaye hivi karibuni ameachia EP yake ya kuitwa "Maturity" ametunukiwa cheti na Recording Academy ambao ni waandaaji wa tuzo za Grammy za nchini Marekani baada ya kushiriki albamu ya msanii kutokea Jamaica wa kuitwa Etana kwenye albamu inayoitwa "Pamoja" ambayo ilitajwa kuwania kipengele cha albamu bora ya reggae.

Katika albamu hiyo  ya "Pamoja" Nandy ameshirikishwa kwenye wimbo uitwao 'Melanin'.  Wasanii wengine walioshirikishwa kwenye album hiyo na wanatarajia kupata vyeti vyao ambao ni Stonebwoy, Vybz Kartel, Alborosie, Patrice, Damian Jr Gong Marley na wengineo.

Ikumbukwe kulingana na utaratibu na sheria za tuzo ya Grammy ni kwamba, ikiwa album itashinda Grammy, basi watu wote walioshiriki kwenye album hiyo kwa maana ya wanamuziki walioshirikishwa, pamoja na waandaaji hupewa cheti maalum cha kutambua mchango wao, cheti ambacho hutolewa na Recording Academy ambao ni waandaaji wa tuzo hizo za Grammy.

[Image Source: Nandy Instagram]

Nandy anaweka historia ya kuwa msanii wa kwanza kutoka Tanzania kupata cheti hicho kutoka waandaaji wa tuzo za Grammy. Kwa Afrika Mashariki, wasanii wengine ambao wana vyeti kutoka Grammy ni pamoja na rapa kutokea Kenya wa kuitwa Kaycyy Pluto pamoja na kundi la Sauti Sol ambalo lilipata tuzo hiyo baada ya kushiriki kwenye albamu ya Burna Boy ya kuitwa "Twice As Tall".

Leave your comment