Rekodi Tano Za Rayvanny Tangu Kuingia WCB Wasafi

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pakua Ngoma Zake Mac Voice Bila Malipo Kwenye Mdundo

Siku chache zimepita tangu mwanamuziki Rayvanny atangaze kuondoka kwenye lebo ya WCB Wasafi ikiwa ni miaka 6 tangu msanii huyo ajiunge na lebo hiyo maarufu hapa Afrika Mashariki. Kupitia WCB Wasafi, Rayvanny aliweza kuachia albamu 1 ya kuitwa Sounds From Africa pamoja na EP nyingine tatu ambazo ni Flowers, Flowers II pamoja na New Chui.

Itoshe kusema kuwa, Diamond Platnumz aliweza kumpika haswa Rayvanny ambaye alianza harakati zake za muziki kwenye kundi la Tip Top Connection na ndani ya miaka yake 6 hapo WCB Rayvanny ameweza kuweka rekodi mbalimbali kwenyw muziki wa nchini Tanzania.

Zifuatazo ni rekodi tano za kimuziki za Rayvanny kipindi akiwa WCB

Tuzo Ya BET

Mwezi Juni mwaka 2017 Tanzania ililipuka kwa furaha baada ya Rayvanny kushinda tuzo ya BET kipengele cha Best International Viewers Choice Awards akiwa ni msanii wa kwanza kutoka Tanzania na wa pili kutoka Afrika Mashariki kushinda tuzo hiyo. Ikumbukwe kuwa Diamond Platnumz ametajwa kuwania tuzo hiyo mara tatu, mara ya mwisho ikiwa ni mwaka 2021 ambapo alipoteza kwa Burna Boy wa Nigeria.

MTV EMA

Mwezi Novemba mwaka 2021 Rayvanny alijiwekea rekodi ya aina yake baada ya kuwa msanii wa kwanza Afrika kutumbuiza kwenye jukwaa la MTV EMA ambapo aliweza kutumbuiza pamoja na msanii Maluma kutokea Columbia wimbo wa "Mama Tetema" ambao ni kama remix ya ngoma yake "Tetema" ambayo aliiachia mwaka 2018.

 Mtandao wa Youtube

Rayvanny pia ni msanii wa pili kutoka Tanzania na Afrika kwa Ujumla  anayeongoza kuwa na wafuatiliaji wengi zaidi kwenye mtandao wa YouTube baada ya Diamond Platnumz. Kufikia sasa Rayvanny amefikisha wafuatiliaji (subscribers) Milioni 3.9 huko Youtube huku akifuatiwa kwa ukaribu na Harmonize ambaye ana subscribers Milioni 3.38.

 Chati Za Billboard

Rayvanny pia anashikilia rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kutokea Afrika Mashariki kuonekana kwenye chati za Billboard Latin kupitia ngoma ya "Mama Tetema" ambayo amemshirikisha Maluma kutoka nchini Columbia ambapo ngoma hiyo iloweza kufika mpaka namba 12 kwenye chati hizo kubwa.

 Gharama Za Video

Hivi karibuni Rayvanny ameweka rekodi ya aina yake baada kuachia video mbili ambazo zote zimegharimu kiasi kikubwa. Video ya "I Miss You" akimshirikisha Zuchu imetajwa kugharimu takriban Milioni 80 za kitanzania huku video ya "Te Quiero" akimshirikisha Marioo ikiwa imegharimu Milioni 100 za kitanzania.

Video ya "Te Quiero" inatajwa kuwa video ya pili kutoka Tanzania kutumia gharama kubwa zaidi ikifuatiwa na  "Nana" ya kwake Diamond Platnumz akiwa na Mr Flavour ambayo inatajwa kugharimu Milioni 92 za, kitanzania.

Leave your comment