Konde Music Worldwide Yafichua Sababu ya Kumuweka Kajala Kuwa Meneja wa Harmonize
7 June 2022
[Picha: Routine Blast]
Mwandishi: Charles Maganga
Pakua Ngoma za Maua Sama Bila Malipo Kwenye Mdundo
Baada ya tetesi kutoka kwa mashabiki na wadau wengine wa muziki nchini Tanzania, hatimaye uongozi wa Konde Music Worldwide, lebo ambayo inaongozwa na mwanamuziki Harmonize imejitokeza hadharani kueleza na kufafanua sababu hasa zilizopelekea Kajala Masanja kuwa moja ya ma-meneja katika lebo hiyo.
Ikumbukwe kuwa siku moja imepita tangu Chopa ambaye ni moja kati ya wasimamizi na viongozi wa lebo ya Konde Music Worldwide kupitia akaunti yake ya Instagram, alitangaza kuwa Kajala Masanja atakuwa ni moja kati ya meneja wa lebo hiyo, tangazo lililosababisha wengi kuhoji kuhusu uamuzi huo.
Soma Pia: Nyimbo Mpya: Diamond ft Mbosso 'Oka', Kayumba 'Baishoo' na Ngoma Zingine Mpya Bongo Wiki Hii
Akizungumza hivi karibuni, akiwa kwenye mahojiano kwenye kituo kimoja cha redio hapa nchini Tanzania, Chopa alithibitisha taarifa hizo kuwa Kajala amepewa cheo cha kuwa Meneja kwenye lebo hiyo na kuongeza kuwa, kwa sasa muigizaji huyo atakuwa ana jukumu la kumsimamia Harmonize pamoja na wasanii wengine kwenye lebo hiyo kama Ibraah, Anjella, Cheed na Killy.
"Ni kweli tumetangaza Kajala ni Meneja na Mkurugenzi pia, kuhusiana na majukumu yake yatakuwa ya kawaida 'as a manager' ni ku-manage shughuli zote za Konde Music Worldwide kuanzia kwa Harmonize mpaka wasanii wengine kama ilivyo sisi kwa ma-meneja wengine” alizungumza Chopa
Kuhusu suala la uzoefu wa Kajala kwenye kiwanda cha muziki, Chopa alisema kuwa Kajala pamoja na kuwa muigizaji, ana uzoefu wa kutosha kwenye muziki na kwamba mwanadada huyo analifahamu vyema soko la muziki hapa nchini Tanzania.
"Kajala sio mgeni, yupo kwenye hii Industry kwa muda mrefu sana hata kama kwa upande wa movie lakini movie na mziki ni vitu vinavyoshabihiana. Ni vitu ambavyo anavijua, ana ique kubwa sana, anaelewa mziki na soko linataka nini na hakuna kitu kigeni kwake," aliongeza Chopa.
Kufikia sasa Kajala anaweka rekodi ya kuwa kati ya wanawake wachache katika tasnia ya muziki wa Tanzania ambao wanasimamia kazi za muziki za wasanii.
Ma-meneja wengine wa kike kutoka Tanzania ni pamoja na Mjerumani ambaye pia anatokea Konde Music Worldwide, Dorice Mziray ambaye ni meneja wa Zuchu pamoja na Christine Mosha maarufu kama Seven ambaye ni Mkurugenzi wa lebo ya Rockstar Africa ambayo kwa sasa inasimamia kazi za Young Lunya, Aslay, Ommy Dimpoz pamoja na Abby Chams.
Leave your comment