Zuchu ‘Sukari’, Vanessa Mdee ‘Closer’ na Nyimbo Zingine za Wasanii wa Kike Tanzania Zilizoweka Rekodi

[Picha: Kenyan Breaking News]

Mwandishi: Charles Maganga

Pakua Nyimbo za Nandy Bila Malipo Kwenye Mdundo

Kwa sasa huwezi kuongelea muziki wa nchini Tanzania bila kuwazungumzia wasanii wa kike ambao mara zote wamekuwa wakifanya bidii kuhakikisha kuwa kiwanda cha muziki nchini Tanzania kinazidi kunawiri. Kuna baadhi ya ngoma kutoka kwa wasanii wa kike wa hapa nchini Tanzania ambazo zimeweka na kushikilia rekodi mbalimbali ambazo hazitakuja kufutika kwenye historia ya muziki hapa nchini.

Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani, zifuatazo ni ngoma tano kutoka kwa wasanii wa kike wa Tanzania ambazo zimeweza kuweka rekodi mbalimbali kwenye muziki wa Bongo Fleva:

Closer - Vanessa Mdee

Vanessa Mdee aliachia ‘Closer Januari 2013 ikiwa ni ngoma ambayo imetayarishwa na Hermy B kutokea studio za B Hitz. Ndani ya wiki moja tu, ngoma hii iliweza kupakuliwa mara (downloads) 30,000 kutoka kwenye mitandao mbalimbali ya kuuza na kutiririsha muziki, kitu ambacho kilikuwa hakijawahi kutokea kabisa kwenye muziki wa Tanzania kwa wakati huo. Aidha ‘Closer’ iliweza kushinda kipengele cha wimbo bora wa R&B mwaka 2014 kwenye tuzo za Kilimanjaro Tanzania Music Awards, kipengele ambacho kwa muda mrefu kilitawaliwa na wanaume.

Elo - Dayna Nyange

Bila shaka ukitaja wasanii wakubwa Afrika huwezi kosa kumtaja Davido; msanii ambaye tangu aanze muziki amefanya kazi na wasanii watatu tu kutoka Tanzania ambao ni Diamond Platnumz, Joh Makini pamoja na Dayna Nyange. Ngoma ya ‘Elo’ ilimfanya Dayna kuwa msanii wa kike wa kwanza kwa Afrika Mashariki kufanya kazi na Davido ambaye ni mshindi wa tuzo za kimataifa ikiwemo BET pamoja na MTV MAMA.

https://www.youtube.com/watch?v=ESHMUhPrO5o

Sukari - Zuchu

Video ya Sukari kutoka kwa Zuchu iliweka rekodi ya aina yake kwa mwaka 2021 baada ya kuwa ndio video ya muziki iliyotazamwa zaidi barani Afrika kwa mwaka wote huo. Aidha, video ya Sukari imeweka rekodi ya kuwa video yenye watazamaji wengi zaidi YouTube kwa nchini Tanzania kwa zile ngoma ambazo msanii amefanya peke yake bila collabo, ikifuatiwa na ngoma ‘Jeje’ ya Diamond Platnumz.

https://www.youtube.com/watch?v=CCmItvVgn6Q

Acha Lizame - Nandy ft Harmonize

Kutokana na watu wengi kusubiri video hii kwa hamu hasa ukizingatia Nandy na Harmonize wote ni wasanii wakubwa, video ya ‘Acha Lizame’ iliweza kufikisha watazamaji Milioni 1 ndani ya masaa 48 tu. Rekodi hii ilimfanya Nandy kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikisha idadi hiyo ya watazamaji kwenye mtandao wa YouTube ndani ya muda mfupi zaidi. Katika kusheherekea rekodi hii, Nandy aliwashukuru mashabiki zake kupitia akaunti yake ya Instagram kwa mara zote kuunga mkono kazi zake anazoziachia.

Rose Muhando - Wanyamazishe

Kutoka kwenye muziki wa Injili, Rose Muhando aliweka rekodi mpya kutoka kwenye wimbo wake wa ‘Wanyamazishe’ ambao ndani yake Rose Muhando ameongelea mambo mengi kumhusu. Video ya ‘Wanyamazishe’ iliweka rekodi ya kuwa ndio wimbo wa Injili uliyotazamwa zaidi nchini Kenya kwa mwaka 2021. Pia wimbo huu ulishika namba 10 kwenye orodha ya nyimbo zilizotazamwa zaidi nchini Kenya kwa mwaka 2021 kwenye mtandao wa YouTube.

https://www.youtube.com/watch?v=wi_Bbsde7Pw

Leave your comment