Rayvanny Kutumbuiza Kwenye Tuzo za MTV EMA Akiwa na Maluma

[Picha: Biggest Kaka]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki kutoka Tanzania Rayvanny amechaguliwa na waandaaji wa tuzo za MTV EMA, kama mojawapo wa wasanii watakaotumbuiza kwenye hafla ya tuzo hizo ambazo zinatarajiwa kufanyika nchini Hungary.

Tuzo hizo za MTV EMA zinatarajiwa kufanyika tarehe 14 Novemba mwaka huu. Inatarajiwa katika hafla hiyo Rayvanny na msanii kutokea Columbia Maluma wataimba wimbo wao mpya kabisa unaoitwa ‘Mama Tetema’ ambao ni remix ya ngoma ‘Tetema’.

Soma Pia: Nyimbo Mpya: Rayvanny Aachia Video ya Ngoma Yake ‘Baila’

Taarifa hizi njema zilitolewa kupitia ukurasa wa Twitter wa MTV EMA ambapo waliandika "Tunathibitisha kuwa Maluma anaachia ngoma mpya wiki hii na atatumbuiza wimbo huo kwa mara ya kwanza kwenye jukwaa la MTV EMA.

Tetesi za ujio wa remix ya ngoma ya ‘Tetema’ baina ya Rayvanny na Maluma zilianza kufuka moshi mwanzoni mwa mwaka huu baada ya Maluma kuchapisha video kwenye akaunti yake ya Instagram iliyomuonesha akicheza ngoma hiyo na marafiki zake.

Maluma aliweka maoni kwenye video hiyo kwa kuandika ‘Remix’ kitu ambacho kwa wengi kiliashiria kuwa Tetema remix iko jikoni.

Kama Rayvanny ataweza kutumbuiza kwenye hafla hiyo, ataweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza kutoka Tanzania kutumbuiza kwenye tuzo za MTV EMA na pia atakuwa ni msanii wa kwanza kutokea Afrika Mashariki kufanya ngoma ya pamoja na Maluma.

Soma Pia: Nyimbo Mpya: Maud Elka na Alikiba Waachia ‘Songi Songi’ Remix [Video]

Maluma ni nani?

Maluma ni gwiji wa muziki kutokea nchini Columbia ambaye kufikia sasa ana albamu nne tangu aanze muziki.

Maluma ameshashirikiana na wasanii wengine wakubwa kama vile Ricky Martin, J Balvin pamoja na The Weeknd. Maluma pia ana wafuasi takriban Milioni 59 kwenye ukurasa wake wa Instagram na mpaka sasa ameshashinda tuzo mbili za Latin Grammy Awards, tuzo mbili za Latin Billboard Music Awards pamoja na nyinginezo nyingi.

Leave your comment