Nyimbo Tano Bora za Hip-hop Kutokea Bongo Zinazogusia Suala la Pesa
31 October 2021
[Picha: Capital News]
Mwandishi: Charles Maganga
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram
Hauhitaji kuwa mhasibu wa benki kufahamu kuwa pesa ni moja kati ya vitu muhimu sana kwenye maisha ya binadamu. Mara nyingi wasio na pesa hutamani kuwa nazo, na walio nazo baadhi yao hupenda kuwatambia wale wasio nazo.
Nchini Tanzania muziki wa Hip-hop ulianza kuwa maarufu mwishoni mwa miaka ya 90 na mwanzoni mwa mwaka 2000. Tangu kuanzishwa kwake, wasanii wa muziki wa Hip-hop wa Tanzania toka kizazi cha kina Sugu na Professor Jay mpaka enzi za sasa za kina Young Lunya na Brian Simba , wasanii wa Hiphop hawajawahi acha kuzungumzia pesa kwenye nyimbo zao.
Soma Pia: Nyimbo Mpya: Rayvanny Aachia EP Mpya ‘New Chui’
Makala hii imelenga kukupitisha kwenye ngoma tano za Hiphop kutoka Tanzania ambazo zimegusia na kuongelea kuhusu pesa.
Soma Pia: Nyimbo Mpya: Lava Lava 'Inatosha', Maua Sama 'Zai' na Ngoma Zingine Zinazovuma Bongo Wiki Hii
Pesa Madafu - Jay Moe
Kwenye ngoma hii, Jay Moe anasisitiza kuwa kama kijana huitaji kuwa na pesa nyingi sana ili uweze kuwa na furaha na kutimiza ndoto yako, unachohitaji ni ‘Pesa Madafu’; ambayo ukiitumia na kuidunduliza vizuri bila shaka utasogea mbele. Kwenye ngoma hii, Jay Mo anatoa faraja na tumaini kwa vijana wanaotafuta pesa waendelee na harakati zao.
Hela - Madee
Kila mtu anapenda pesa lakini je ukishaipata ya kutosha utakuwaje? Hilo ni swali ambalo Madee anajaribu kulitatua kwenye ngoma hii. Madee anaonesha namna ambavyo pesa inaondoa uaminifu, inapora haki za watu, na kusababisha watu kukosa heshima kwa wakubwa zao.
Money - AY
Kama binadamu kuna siku unaamka asubuhi na unakosa kabisa mwamko wa kufanya kazi. Kwa kulitambua hilo, ndio maana AY miaka kadhaa nyuma aliachia ngoma ya ‘Money’ ambayo ndani yake anawapa vijana hasira, mwamko na hamasa ya kutafuta pesa ili waweze kuishi kama wafalme siku za usoni.
Dume Suruali - Mwana FA ft Vanessa Mdee
Huu ni wimbo ambao unajaribu kugusia suala zima la mahusiano na pesa. Mwana FA anaweka wazi msimamo wake kuwa hawezi kumuhonga mwanamke pesa ili apate mapenzi, kitu ambacho Vanessa Mdee kwenye wimbo huu anakipinga vikali na anaamua kumuita Mwana FA ‘Dume suruali’ kwa kuwa hampi pesa .
Kwenye ngoma hii Mwana FA aliwasemea wanaume wengi ambao wanadharaulika kutokana na kutowahudumia wanawake zao, ambao mara nyingi hupenda vitu vya thamani.
Pesa - Mr Blue
Waswahili wanasema tumia pesa ikuzoee na Mr Blue alizidi kukoleza usemi huo kupitia ngoma yake ya ‘Pesa’ aliyomshirikisha Becka.
Huu ni wimbo ambao Mr Blue anasheherekea na kufurahi na marafiki zake baada ya kutafuta pesa kwa muda mrefu. Kama wewe ni mtafutaji, basi ngoma hii itakufaa sana kipindi cha mapumziko yako.
Leave your comment