Tanasha Donna Azungumzia Kukataa Kushiriki Kwenye Video ya Diamond

[Picha: Diamond Instagram]

Mwandishi: Brian Sikulu

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mwanamuziki nyota kutoka Kenya Tanasha Donna amefichua kuwa alikataa ombi la msanii Diamond Platnumz la kumtaka kutokea katika video ya wimbo wake wa 'Naanzaje'.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusikiliza albamu ya msanii maarufu Alikiba iliyofanyika nchini Kenya, Tanasha alikiri kuwa alipokea ombi hilo ila kwa sababu ambazo hakuzifichua, alilikataa.

Soma Pia: Diamond Platnumz Atuzwa Msanii Bora wa Afrika

 Tanasha ni mpenzi wa zamani wa msanii Diamond na walibarikiwa na mtoto wa kiume wakati wa mahusiano yao. Wawili hao pia wamewahi kufanya kazi pamoja na kushirikiana kwenye wimbo wa 'Gere', ambao kufikia sasa umetazamwa takriban mara milioni ishirini na saba kwenye mtandao wa YouTube.

Uamuzi wa Tanasha Donna kukataa kutokea kwenye video ya Diamond Platnumz umeibua hisia tofauti mtandaoni. Tanasha Donna kwa siku za hivi karibuni ameonekana kuwa na ukaribu mno na msanii Alikiba ambaye ni mpinzani mkuu wa Diamond Platnumz.

Soma Pia: Rais Samia Suluhu Awapongeza Wasanii wa Bongo Waliotajwa Kuwania Tuzo za AFRIMA

Zaidi ya urafiki, Tanasha Donna na Alikiba pia wanafanya kazi pamoja chini ya kampuni ya usambazaji wa muziki iitwayo Ziiki Media. Huenda ni ukaribu huu wa wasanii hawa wawili ambao umezalisha kolabo baina ya Tanasha Donna na msanii chipukizi Tommy Flavour ambaye amesainiwa katika lebo ya Kings Music.

Picha na video zimeibuka mitandaoni zikimwonyesha Tanasha Donna wakati wakirekodi video ya kolabo yake na Tommy. Ngoma hiyo itakuwa katika albamu ya Tommy Flavour ambayo inatarajiwa kutoka baadae mwakani.

Leave your comment