Mkubwa Fella Azungumzia Kuvunjika kwa Yamoto Band, Ukimya wa Aslay
4 October 2021
[Picha: Mkubwa Fella Instagram]
Mwandishi: Brian Sikulu
Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram
Mkubwa Fella ambaye kwa sasa ni meneja wa mwanamuziki nyota nchini Tanzania Mbosso amefunguka kuhusu kuvunjika kwa kundi la Yamoto Band. Fella ndiye alianzisha kundi la Yamoto Band ambalo lilikuwa na wanachama wanne, Mbosso akiwa mmoja wao.
Kundi hilo, hata hivyo, baada ya kupata umaarufu na mafanikio makubwa lilivunjika huku kila msanii akienda zake na kufanya kazi kama mwanamuziki huru.
Mbosso alibaki chini ya usimamizi wa Mkubwa Fella kupitia lebo ya WCB huku wenzake wakiwemo Aslay, Beka Flavour na Enock Bella wakichukua mkondo mwingine.
Soma Pia: Mkubwa Fella Afunguka Kuhusu Bendi Mpya ya New Yamoto Band
Akizungumza katika mahojiano ya hivi karibuni, Mkubwa Fella alikiri kuwa kundi hilo lilivunjika kwa sababu ya ukuaji wa wanachama wake. Alieleza kuwa huenda wasanii hao wanne walitaka kukuwa zaidi na pia kupata mafanikio ya kibinafsi, na hivyo basi wakalazimika kuliaga Yamoto Band. "
Labda mimi nizungumze kwamba ukuaji, kuwa wakubwa zaidi wameenda kujitafutia zaidi. Lakini ule mmoja bado niko naye, Maromboso bado nko naye. Wengine walienda kutafuta," Mkubwa Fella alisema.
Soma Pia: Beka Flavour Apongeza Mkubwa Fella kwa Kuanzisha New Yamoto Band
Aidha, Fella alizungumzia ukimya mrefu wa msanii Aslay. Aslay amekuwa kimya kwa muda mrefu na mashabiki wake wanahofia kuwa huenda nyota yake katika tasnia ya muziki ikafifia.
Kwa mujibu wa Fella, Aslay anajipanga ili arudi tena. Aliongeza kuwa yeye kibinafsi hangependa kumwona Aslay akididimia na kupotea kimuziki.
"Nikisema kwamba amepotea, akiwa napotea roho itaniuma. Lakini akiwa anajipanga mimi naona kweli anajipanga na mimi napenda. Lakini akiwa ndio kakaa kimya alimuradi ati anapotea, pale kidogo nitaona kwa nini apotee. Lakini kama anajipanga, ni vizuri," Mkubwa Fella aliongezea.
Leave your comment