Mac Voice Ajibu Madai ya Kumuiga Rayvanny Kwenye Uimbaji Wake

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Charles Maganga

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Nyota mpya kutokea lebo ya Next Level Music Mac Voice amefunguka kuhusu kauli za mashabiki, ambao aghalabu wamekuwa wakimshtumu kuwa aina yake ya kufanya muziki inafanana sana na bosi wake Rayvanny.

Tangu atoe EP yake ya ‘My Voice’ siku chache nyuma, mashabiki wengi mtandaoni wamekuwa wakifananisha sauti, uwezo wa kuimba pamoja na midondoko ya msanii huyo na Rayvanny.

Kupitia mahojiano aliyoyafanya kwenye The Switch hivi karibuni, msanii huyo amekanusha kumuiga Rayvanny.

Soma Pia: Nyimbo Mpya: Mac Voice Aachia EP Mpya ‘My Voice’ Chini ya Next Level Music

"Mimi nafikiri kwa sababu ni mpya masikioni mwao na nikiendelea kusikika kadri wanavyoendelea kunisikia watagundua kuwa mimi nina kitu changu na brother Rayvanny ana kitu chake. Nadhani kwa sababu ni mpya ndo mana unakuta wananifananisha," alizungumza msanii huyo.

Rayvanny ambaye alisindikizana na msanii huyo alikoleza zaidi utetezi wa msanii wake, kwa kusema kuwa watanzania wampe muda zaidi msanii huyo na wakimsikilize kwa muda mrefu zaidi watafahamu utofauti wake kwenye sauti.

"Kwenye muziki within one melody there are other 100 melodies watu waendelee kumpa sikio voice ana tone yake, ukimsikiliza vizuri utajua kabisa huyu ni Mac Voice alafu huyu ni Chui," alizungumza Rayvanny.

Soma Pia: Nyimbo Mpya: Mac Voice Aachia Video ya 'Nenda'

Aidha, Rayvanny alisema kuwa sababu kubwa ya kumkubali Mac Voice kwenye lebo yake ya Next Level Music ni kuwa msanii huyo ana kipaji kikubwa sana cha muziki, ikiwemo uwezo mkubwa wa kubadilika kwenye kila wimbo anaoufanya.

Kwa sasa, Mac Voice anatamba na EP yake ya ‘My Voice’ ambayo imesheheni nyimbo sita.

Leave your comment