Harmonize Ahairisha Utambulisho wa Cheed Huku Rayvanny Akimpigia Mac Voice Kampeni

[Picha: Instagram]

Mwandishi: Brian Sikulu

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Mkurugenzi mkuu wa lebo ya Konde Music Worldwide Harmonize ametangaza kuhairishwa kwa utambulisho wa msanii chipukizi Cheed.

Cheed alikuwa ameratibiwa kuachia ngoma yake ya kwanza chini ya usimamizi wa Konde Music tarehe 24 mwezi huu. Kwa mujibu wa Harmonize, usimamizi wa Konde Music umelazimishwa kusitisha utambulisho huo kwa sababu zilizozidi uwezo wao.

Soma Pia: Rayvanny ‘Wanaweweseka’, Jux ‘Sina Neno’ na Nyimbo Zingine Zinazotamba Bongo

Harmonize hata hivyo hakufichua uhairisho huo utakuwepo kwa muda wa siku ngapi. Aliwaahidi mashabiki wake kuwa watatangaza tarehe rasmi ya Cheed kutoka. "Siku zote mwenye subira bila shaka yupo karibu na Mungu. Najua kwa kiasi gani mnamsubiri Cheed ila ningependa kuchukua nafasi hii kuwataarifu kwamba kwa sababu zilizopo kando ya uwezo wetu Cheed Day haitokuwepo tarehe 24/09/2021 kama tulivyopanga hapo awali. Tunawaahidi kuwajuzalini na siku gani hivi punde," chapisho la Harmonize mtandaoni lilisomeka.

Kwa upande mwingine, rais wa lebo ya Next Level Music Rayvanny amezidisha kampeni za kumtabulisha msanii wake wa kwanza ambaye ni Mac Voice.

Soma Pia: Diamond Platnumz, Zuchu, Nandy Alikiba, Darassa, Harmonize na Rayvanny Watajwa Kuwania Tuzo Za AFRIMA 2021

Mac Voice anatarajiwa kutambulishwa rasmi hii leo tarehe 24 ndani ya Wasafi TV na vile vile kupitia akaunti yake ya YouTube mwendo wa saa moja jioni.

Aidha, imekisiwa kuwa huenda msanii huyo akaachia ngoma yake ya kwanza katika uzinduzi huo.

"Uvumilivu , maombi na kujituma ni siri ya mafanikio. Umekua msikivu lakini Pia mvumilivu na unaejituma sana naamini ndoto yako nikuona unafanikiwa na kuleta japo tabasamu kwenye familia yako. Wengi wetu tunatoka familia duni Sana vipaji Mungu alivyotupa ndivyo tunategemea vitukomboe katika maisha yetu. Nichukue nafasi hii kukuomba mdau wa mziki na unaesapoti vijana wapambani kutushika mkono ili tuzidi kutimiza ndoto na kulitangaza taifa duniani," Rayvanny aliandika mtandaoni.

Leave your comment