Beka Flavour Afichua Sababu Kuu Iliyofanya Yamoto Band Kuvunjika

[Picha: Hivisasa]

Mwandishi: Brian Sikulu

Pata Habari za Muziki na Mixtapes Bure Kwenye Telegram

Msanii mahiri kutokea nchini Tanzania Beka Flavour amejitokeza na kuelezea sababu kuu iliyosababisha kundi la Yamoto Band kuvunjika. Beka Flavour pamoja na wasanii wenzake ambao ni Aslay, Enock Bella na Mbosso walikuwa wanachama wa kundi hilo ambalo kwa wakati huo lilivuma sana na miziki zao za kusisimua.

Kuvunjika kwa kundi hilo kulikuwa pigo kubwa sana kwa mashabiki ambao walikuwa wakienzi jinsi wasanii hao wanafanya kazi kwa pamoja.

Akizungumza katika mahojiano na Simulizi Na Sauti, Beka Flavour alikana madai kuwa tofauti baina yao ndiyo iliyosababisha kuvunjika kwa bendi hiyo. Alifafanua na kueleza kuwa walilazimika kufanya kazi kama wasanii huru kwa sababu za kimaslahi.

Kulingana na Beka Flavour, kipato walichokipata kilikuwa kidogo haswaa baada ya kugawa baina ya wanachama na pia kuwalipa wasimamizi wao. Hivyo basi, walifanya mkutano kama wanachama wa kundi hilo na kukubaliana kuiaga bendi ya Yamoto kwaheri.

Beka Flavour alisisitiza kuwa wanachama wote wako sawa na hawakukosana wala kuachana kwa ubaya. Isitoshe, wasanii hao wanne hadi leo bado wangali marafiki na wanatembeleana mara kwa mara.

Aliongeza kuwa msimamizi wao kwa wakati huo ambaye alikuwa ni Mkubwa Fella alijaribu kuwaunganisha tena lakini aliambulia patupu, kwani maji yalikuwa yashamwagika.

"Sababu ni hiyo hiyo tu maslahi. Sana sana ni maslahi. Sisi wenyewe tuliona kuwa sasa tulipofikia kila mmoja anaweza akafanya muziki wake mwenyewe, na akatengeneza families zake mwenyewe, na akaendelea kupata kipato mwenyewe ambacho hakitakuwa na mambo mengi," Beka Flavour alieleza.

Leave your comment